" MHANDISI JAMES JUMBE ASIFU UTEKELEZAJI WA MIRADI KIPINDI CHA RAIS SAMIA, ACHANGIA MIFUKO 100 YA SARUJI KWA KITUO CHA AFYA KAMBARAGE

MHANDISI JAMES JUMBE ASIFU UTEKELEZAJI WA MIRADI KIPINDI CHA RAIS SAMIA, ACHANGIA MIFUKO 100 YA SARUJI KWA KITUO CHA AFYA KAMBARAGE

Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya CCM wilayani humo Mhandisi James Jumbe akizungumza.

Na Mapuli Kitina Misalaba

 Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya CCM wilayani humo Mhandisi James Jumbe, amesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amefanikisha maendeleo makubwa katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake.

Akizungumza katika ziara ya Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga mjini, Mhandisi Jumbe ameeleza kuwa maendeleo haya yameonekana katika sekta mbalimbali ikiwemo ujenzi wa Daraja la Busisi, reli ya kisasa ya SGR, viwanda, miundombinu, afya, mahusiano ya kimataifa, ukuaji wa uchumi, na usuluhishi wa migogoro.

“Rais Samia ameonesha uzalendo wa hali ya juu katika kusukuma maendeleo ya nchi yetu. Tumeshuhudia utekelezaji wa miradi mikubwa kama Bwawa la Mwalimu Nyerere, ambayo siyo tu inahitaji rasilimali kubwa bali pia inahitaji ujuzi wa hali ya juu kuitekeleza kwa mafanikio,” amesema Mhandisi Jumbe.

Ameongeza kuwa katika suala la ukusanyaji wa mapato na kodi, serikali ya Rais Samia imefanikiwa kuimarisha mifumo, hali ambayo imeongeza mapato ya taifa na kuwezesha utekelezaji wa miradi mikubwa kwa wakati.

“Kasi ya maendeleo ni kubwa na hakuna mradi uliokwama licha ya changamoto mbalimbali. Mama Samia ameonesha kuwa ni kiongozi mwenye maono, uwezo wa kusimamia miradi, na anatekeleza mipango yake kwa kasi kubwa kwa manufaa ya wananchi wote,” amesema Jumbe.

Mhandisi Jumbe amewahamasisha wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla kuendelea kumuunga mkono Rais Samia pamoja na mgombea mwenza wake Dkt. Emmanuel Nchimbi, akibainisha kuwa ni viongozi makini wenye uwezo mkubwa wa kusimamia maendeleo ya nchi.

“Kama chama, tumepewa wagombea makini. Dkt. Emmanuel Nchimbi ni mbobezi katika uongozi, siasa na mahusiano ya kimataifa, na Dkt. Hussein Mwinyi ameleta maendeleo makubwa Zanzibar. Kwa hiyo, ni wakati wa kuendelea kuwaunga mkono viongozi hawa,” amesemaJumbe.

Aidha Mhandisi James Jumbe Wiswa pia amekabidhi mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa uzio katika Kituo cha Afya Kambarage, Manispaa ya Shinyanga.

Mchango huo unalenga kuimarisha usalama wa wagonjwa, hususan akina mama na watoto wachanga wanaopatiwa huduma katika kituo hicho.

Akizungumza wakati wa makabidhiano, Mhandisi Jumbe amesema ametoa msaada huo kama sehemu ya kutimiza ahadi yake ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha sekta ya afya.

"Nimeamua kutimiza ahadi yangu ya kusaidia ujenzi wa uzio wa Kituo cha Afya Kambarage ili kuhakikisha mazingira salama kwa wagonjwa, hususan akina mama na watoto wanaopata huduma hapa. Kamati ya Kituo hiki ilileta ombi, nami nikaona ni muhimu kulitekeleza kwa vitendo," amesema Mhandisi Jumbe.

Ameeleza kuwa mchango huo ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kuboresha sekta ya afya kwa kuhakikisha vituo vya afya vinakuwa na miundombinu bora na salama.

“Rais Samia amejitahidi kuimarisha sekta ya afya kwa kuleta vifaa tiba vya kisasa na kuboresha huduma. Sisi kama wadau wa maendeleo tunapaswa kushiriki katika kuunga mkono juhudi hizi. Nawaomba wafanyabiashara wa Shinyanga pia waone umuhimu wa kuchangia miradi ya maendeleo,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Kituo cha Afya Kambarage, Adolf Nzwanzungwanko, ameushukuru mchango huo na kueleza kuwa utasaidia kuimarisha usalama wa kituo hicho, hususan nyakati za usiku.

Naye Mganga Mfawidhi wa Kituo hicho, Dkt. Ernest Magula, amesema ujenzi wa uzio huo utaongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa na kupunguza changamoto ya watu wasiokuwa na mahitaji ya kitabibu kuzurura ndani ya eneo la hospitali.

Katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mzee Fue Mrindoko, pamoja na mambo mengine ameahidi kuwa jumuiya hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi zote za maendeleo zinazotekelezwa chini ya Ilani ya CCM.

Naye Katibu wa Jumuiya hiyo, Bi Doris Yotham Kibabi, amewahamasisha viongozi wa jumuiya hiyo katika ngazi za kata, matawi na mashina kuongeza wanachama wapya ili kukiimarisha chama.

Jumuiya ya Wazazi ya CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini leo Februari 22, 2025 imefanya ziara zake katika kata za Kambarage, Lubaga, na Mjini kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhimiza mshikamano miongoni mwa wanachama.


Post a Comment

Previous Post Next Post