Na Mapuli Kitina Misalaba
Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linamshikilia mwanamke mmoja anayefahamika kwa jina la Sai Charles (38) mkazi wa Mwakitolyo, kwa tuhuma za kumuiba mtoto mchanga wa siku moja kutoka kwa mama yake mzazi Rahel Mathayo (19), mkazi wa Bulige.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi Janeth Magomi amesema tukio hilo limetokea mnamo Februari 5, 2025, majira ya saa moja usiku katika Kijiji na Kata ya Bulige, ambapo mama huyo aligundua kuwa mtoto wake ametoweka mara baada ya kuoga.
Kwa mujibu wa taarifa za Jeshi la Polisi, mtuhumiwa alijitokeza katika Zahanati ya Ngaya, Wilaya ya Kipolisi Msalala, muda mfupi baada ya Rahel kujifungua. Akijifanya ndugu au rafiki wa karibu, Sai alijitwika jukumu la kumsaidia mama huyo mchanga, akijenga urafiki wa karibu naye.
Baada ya Rahel kuruhusiwa kutoka Zahanati na kurejea nyumbani, mtuhumiwa aliendelea kumsaidia kwa kumbeba mtoto hadi nyumbani kwao Bulige. Hata hivyo, alipofika huko, Rahel aliingia bafuni kuoga, na aliporejea hakumkuta mtoto wake pamoja na mtuhumiwa huyo.
Baada ya kugundua kuwa mtoto wake ameibwa, Rahel alipiga yowe na kuomba msaada ambapo vijana wa bodaboda waliokuwa karibu walitoa taarifa muhimu kwa polisi, wakieleza kuwa mtuhumiwa alikuwa amepanda bodaboda kuelekea Mwakitolyo akiwa na mtoto mchanga.
Kwa kutumia taarifa hizo, Jeshi la Polisi limefanya msako wa haraka na kufanikiwa kumkamata Sai Charles katika Kata ya Mwakitolyo akiwa na mtoto huyo, ambaye tayari amerudishwa salama kwa mama yake mzazi.
Katika mahojiano ya awali na polisi, Sai Charles amedai kuwa alikuwa na watoto wakubwa lakini alitamani kupata mtoto mchanga mwingine, jambo ambalo halikuwezekana kwa njia ya kawaida ndiyo maana alifikiria kuchukua mtoto wa mwingine ili awe wake.
Kamanda Magomi amepongeza juhudi za wananchi, hususan waendesha bodaboda, kwa kutoa taarifa zilizosaidia kufanikisha kukamatwa kwa mtuhumiwa.
"Jeshi la Polisi linawashukuru sana vijana wa bodaboda kwa ushirikiano wao bila wao, huenda mtuhumiwa angefanikiwa kutokomea na mtoto huyo, tunawahimiza wananchi wote kuendelea kushirikiana nasi katika kukabiliana na uhalifu wa aina hii," amesema Magomi
SACP Magomi amewataka wananchi, hususan wanawake, kuwa waangalifu na watu wanaojitokeza kujifanya ndugu au marafiki baada ya kujifungua huku akiwatahadharisha kuwa wizi wa watoto ni kosa la jinai na kwamba hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayejihusisha na vitendo hivyo.
"Wizi wa mtoto siyo jambo dogo ni kosa kubwa la jinai tunawataka wananchi wote kuwa makini na kufuata maadili ya Kitanzania, badala ya kutafuta watoto kwa njia zisizohalali," amesema Magomi
Kwa sasa, mtuhumiwa Sai Charles anashikiliwa na Jeshi la Polisi na anatarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya upelelezi wa awali kukamilika.
Post a Comment