" RAIS SAMIA ATAMBULIWA KAMA KINARA WA AJENDA YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA BARANI AFRIKA

RAIS SAMIA ATAMBULIWA KAMA KINARA WA AJENDA YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA BARANI AFRIKA



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea kuonesha uongozi thabiti katika masuala ya mabadiliko ya tabianchi na nishati endelevu kwa bara la Afrika. Katika kikao cha pembezoni cha Kamati ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (CAHOSSCC) kilichofanyika Addis Ababa, Ethiopia, Rais Dkt. Samia aliwasilisha Azimio la Dar es Salaam, akisisitiza umuhimu wa Afrika kushiriki kikamilifu katika mijadala ya kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Bi. Shirika Nyanga imesema Kikao hicho, kilichoongozwa na Mwenyekiti wa CAHOSSCC, Rais wa Kenya Mhe. William Ruto, kiliridhia Azimio la Dar es Salaam kuwasilishwa kwa Baraza la Umoja wa Afrika kwa ajili ya kupitishwa. Azimio hilo lilipitishwa bila kupingwa, hatua inayodhihirisha mshikamano wa Afrika katika kutetea maslahi yake kuhusu tabianchi na nishati endelevu.

Katika hatua nyingine muhimu, Rais Dkt. Samia aliwasilisha ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia, ambayo ilipendekezwa na Tanzania, akibainisha kuwa nishati hiyo ni hitaji muhimu kwa zaidi ya watu milioni 900 barani Afrika wanaokosa fursa ya kuitumia. Uwasilishaji wake uliungwa mkono kwa nguvu na Baraza la Umoja wa Afrika, ambalo limemtambua na kumpongeza Rais Dkt. Samia kama kinara wa ajenda hiyo barani Afrika.

Kwa kutambua mchango wake mkubwa katika masuala ya nishati na tabianchi, Mkutano wa 38 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliofanyika Februari 15, 2025, ulimchagua Rais Dkt. Samia kuongoza Tanzania kama mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Umoja wa Afrika kwa mwaka 2025. Tanzania itawakilisha Kanda ya Mashariki kama Makamu wa Tatu wa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, nafasi inayothibitisha ushawishi wake katika siasa na maendeleo ya bara hili.

Tanzania inajiunga na nchi nyingine katika Kamati hiyo, zikiwemo Angola (Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika 2025) kutoka Kanda ya Kusini, Burundi (Makamu wa Kwanza wa Mwenyekiti) kutoka Kanda ya Kati, na Ghana (Makamu wa Pili wa Mwenyekiti) kutoka Kanda ya Magharibi, huku Mauritania, iliyokuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika kwa mwaka 2024, ikiteuliwa kuwa Katibu wa Kamati hiyo.

Hatua hizi zinaonesha kwa mara nyingine nafasi muhimu ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuongoza mijadala na utekelezaji wa sera za maendeleo endelevu barani Afrika.

Post a Comment

Previous Post Next Post