Na Mapuli Kitina Misalaba
Serikali kupitia Wizara ya Afya imekanusha uvumi unaoenea mitandaoni kuhusu uhaba wa dawa za kufubaza makali ya Virusi vya UKIMWI (ARV) na kuwataka wananchi kupuuza taarifa hizo.
Kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa, Februari 8, 2025, Wizara ya Afya imeeleza kuwa hakuna uhaba wa dawa hizo na kwamba zinapatikana kwa wingi kwa watumiaji wake.
Aidha, wizara hiyo imebainisha kuwa taarifa za upotoshaji zimewafanya baadhi ya wagonjwa kuomba dawa kwa muda mrefu kwa ajili ya akiba, hali inayoweza kuathiri usambazaji na matumizi sahihi ya dawa hizo. Serikali imewasihi wananchi kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa afya ili kuepuka usugu wa dawa na madhara mengine ya kiafya.
Wizara ya Afya pia imewataka wananchi kuwa makini na taarifa zisizo sahihi kuhusu afya zinazosambazwa mitandaoni na kuhakikishia kuwa huduma za dawa za ARV zinaendelea kupatikana bila tatizo lolote.
Post a Comment