" SUNGUSUNGU WALIOMJERUHI MTU KWA KIPIGO WANASWA NA POLISI

SUNGUSUNGU WALIOMJERUHI MTU KWA KIPIGO WANASWA NA POLISI


Siku chache baada ya mkazi wa Kijiji cha Mbika kata ya Ushetu Wilayani Kahama mkoani Shinyanga aliyejulikana kwa jina la John Julius (34), kupigwa na walinzi wa jadi (sungusungu) kwa madai ya wizi wa mlango wa mwanakijiji mwenzake, jeshi la polisi mkoani humo limesema linawashikilia watu wawili kwa tuhuma hizo. Kamanda wa polisi mkoani humo SACP Janeth Magomi amewataja wanaoshikiliwa kwa ukatili huo kuwa ni Bundala Dalali na Issack Kulwa ambao ni walinzi wa jadi, na kwamba upelelezi wa tukio hilo bado unaendelea na utakapo kamilika watafikishwa mahakamani. "Tunawashikilia Watuhumiwa wawili ambao ni Bundala Dalali na Issack Kulwa kwa kuhusika na tukio hili na upelelezi unaendelea tukikamilisha tutawafikisha Mahakamani,niwaombe Wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na kama mtu amekamatwa kwa tuhuma ya wizi ni bora akafikishwa polisi,"alisema Magomi. Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, akiwemo Magema Kafuku, alisema John alishambuliwa na Walinzi wa Jadi (Sungusungu) baada ya kutuhumiwa kuiba mlango wa Mwajiri wake aliyefahamika kwa jina la Mwajuma Haruna, kwa kupigwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake. Aliendelea kueleza kuwa John alifikia hatua ya kung'oa mlango wa nyumba ya Mwajuma aliyempa kibarua cha kulima shambani baada ya mwajiri wake huyo kushindwa kumlipa ujura wake wa shilingi elfu ishirini (20,000) walizokubaliana. Akizungumzia tukio hilo Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbika Benedicto Mlangani, alisema kuwa alipokea taarifa za kupigwa kwa John Febuari 15 akituhumiwa kuiba Mlango huku akiwa hoi hajitambui na alielekeza apelekwe katika kituo cha afya Ushetu ili kunusuru uhai wake. "Tumebaini John alipigwa kimakosa walikuwa wanadaiana fedha na Mwajiri wake Mwajuma ambaye kwa sasa tunamshikilia ili aweze kugharamia matibabu yake, lakini walipaswa kumfikisha ofisini kwangu na sio kumuadhibu,"alisema Mlangani. Mganga Mfawidhi wa Kituo cha afya Ushetu Dk William Msigale, alikiri kumpokea John Febuari 16 Mwaka huu akiwa na Majeraha katika sehemu mbalimbali za mwili wake, na kumpatia matibabu, na kwamba kwa sasa wanampa rufaa kwenda Hospitali ya Halmashauri ya Ushetu kupiga X ray kutokana na mguu wake kuonekana una mvunjiko. Nae Mhanga wa tukio hilo John Julius Mkazi wa Kijiji cha Mbika, akielezea tukio hilo akiwa amelazwa katika kituo cha afya Ushetu alisema kuwa alipigwa na Sungusungu baada kuchukua mlango wa Mwajiri wake Mwajuma Haruna kwa makubaliano yao wawili, baada kushindwa kumlipa elfu ishirini (20,000)kama ujira wake baada ya kumlimia shamba lake. "Tulikubaliana nichukue Mlango akipata hela atakuja kuukomboa, lakini nilipouchukua alipiga kelele za Mwizi ndipo Sungusungu wakaja wakaniadhibu kwa kunipiga sana kama mwizi na mafimbo,"alisema Julius.

Post a Comment

Previous Post Next Post