Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga Frank Habibu Mahimbali akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini, yaliyofanyika leo Februari 3, 2025, katika viwanja vya mahakama hiyo.
Na Mapuli Kitina Misalaba
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga,
Frank Habibu Mahimbali, amewasihi mahakimu kutekeleza majukumu yao kwa kufuata
viapo vyao bila upendeleo au chuki, akisisitiza kuwa maamuzi yao yanapaswa kuwa
suluhisho la migogoro inayowasilishwa mahakamani badala ya kuzidisha matatizo
katika jamii.
Akizungumza kwenye kilele cha maadimisho ya wiki ya
sheria leo Februari 3, 2025 Jaji Mahimbali ameeleza kuwa migogoro inayofikishwa
mahakamani ni halisi, hivyo ni wajibu wa mahakimu kuhakikisha kuwa wanatoa
maamuzi yenye haki na yanayosaidia katika kutatua migogoro hiyo kwa ufanisi.
“Kukengeuka
na viapo vyetu ni sawa na uasi wa kazi. Tunaelekea robo ya pili ya karne ya 21,
tunapaswa kuwa sehemu ya suluhisho na siyo chanzo cha matatizo zaidi. Niwasihi
sana waheshimiwa mahakimu tuonyeshe umahiri wetu kisheria katika utatuzi wa
migogoro,” amesema Jaji Mahimbali.
Aidha, ametoa rai kwa taasisi zote za haki madai
kuwa na mpango mkakati madhubuti wa utekelezaji wa sera na utoaji wa huduma kwa
wananchi kwa ufanisi zaidi.
Jaji Mahimbali amesisitiza umuhimu wa kuwa na
watumishi waadilifu na wanaoheshimu utawala wa sheria, pamoja na kuimarisha
mifumo ya TEHAMA ili kurahisisha utendaji wa Mahakama.
Jaji Mahimbali pia amewasilisha takwimu za mashauri
yaliyosajiliwa na kusikilizwa katika Kanda ya Shinyanga kwa mwaka 2024,
akifafanua kuwa hali ya ufunguaji na usikilizaji wa mashauri ilikuwa kama
ifuatavyo:
Jumla ya mashauri mapya yaliyofunguliwa mwaka 2024 yalikuwa
11,988.
Mashauri yaliyokuwa yamesalia kutoka mwaka 2023
yalikuwa 1,349.
Katika mwaka 2024, jumla ya mashauri 12,175
yalisikilizwa, na yaliyobaki kufikia mwishoni mwa mwaka yalikuwa 1,216.
Kwa Mahakama Kuu pekee, mashauri 783 yalifunguliwa,
huku 1,009 yakisikilizwa na kubaki mashauri 239.
Jaji Mahimbali amebainisha kuwa kasi ya usikilizaji
wa mashauri imeongezeka, akitoa mfano wa Mahakama Kuu ambayo ilisikiliza
mashauri 914 mwaka 2023, na mwaka 2024 mashauri 1,009 yalisikilizwa, ikiwa ni
ongezeko la asilimia moja.
“Kwa
mahakama kuu, tumefanikiwa kumaliza mashauri ya mrundikano kutoka 33 mwaka 2023
hadi 0 mwaka 2024. Kufikia Desemba 31, 2024, tulikuwa tumekamilisha mashauri
yote ya 2023, isipokuwa mashauri mawili pekee ambayo yako kwenye rufaa Mahakama
ya Rufani,” amesema Jaji Mahimbali.
Jaji Mahimbali ameongeza kuwa maamuzi yote ya
mashauri 1,009 yaliyosikilizwa katika Mahakama Kuu mwaka 2024 yamehifadhiwa
kwenye mfumo wa kuhifadhi nakala laini za hukumu kwa ajili ya kumbukumbu na
upatikanaji wa haraka wa taarifa.
Jaji Mahimbali amewashukuru wadau wa Mahakama kwa
ushirikiano wao mkubwa katika kuhakikisha kuwa haki inatendeka kwa wakati na
kwa ufanisi ambapo ameeleza kuwa mafanikio yaliyopatikana ni matokeo ya juhudi
za pamoja kati ya Mahakama na wadau wake wote.
Mmoja wa wananchi ameiomba Mahakama kuendelea
kutenda haki na kuhakikisha kuwa mashauri yanamalizika kwa wakati ili kuepusha
ucheleweshaji wa haki.
Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya
Shinyanga, Caccelini Shaban Langau, amehakikishia wananchi kuwa Mahakama
itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi na kasi inayotakiwa.
Leo ni siku ya kilele cha maadhimisho ya wiki ya
sheria nchini ambapo Mahakama Kuu kanda ya Shinyanga imetoa mwanga wa kuhakikisha
kuwa haki inatendeka kwa uwazi na ufanisi, huku jitihada za kupunguza
mrundikano wa mashauri zikiendelea kuzaa matunda.
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali serikali, vyama vya siasa, taasisi binafsi pamoja na mwakilishi wa mkuu wa Mkoa wa Shinyanga ambaye ni mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Wakili Julius Mtatiro.
Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Wiki ya Sheria mwaka 2025 ni: "Tanzania ya 2050: Nafasi ya Taasisi Zinazosimamia Haki Madai katika Kufikia Malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo."Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda
ya Shinyanga Frank Habibu Mahimbali akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya
Sheria nchini, yaliyofanyika leo Februari 3, 2025, katika viwanja vya mahakama
hiyo.