Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Donasian Kessy akitoa taarifa yake kwa waandishi wa habari leo Februari 4, 2025.
Na Mapuli Kitina Misalaba
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
Mkoa wa Shinyanga imefanikiwa kuokoa shilingi milioni 137.8 ikiwa ni sehemu ya
fedha za malipo ya mauzo ya viwanja 29 vilivyopimwa na Manispaa ya Kahama mwaka
2019.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Donasian Kessy,
ametoa taarifa hiyo leo wakati akielezea utekelezaji wa majukumu ya taasisi
hiyo kwa kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2024/2025, kuanzia Oktoba
hadi Desemba.
Amesema Manispaa ya Kahama ilikuwa ikimiliki ardhi
katika eneo la Phantom na mwaka 2019 iliamua kupima na kuuza viwanja hivyo kwa
wananchi. Hata hivyo, amesema TAKUKURU inaendelea kufuatilia malipo ya fedha
zilizobaki, ambazo ni zaidi ya shilingi milioni 600.
“Mwaka
2024, TAKUKURU kupitia vyanzo vyake vya siri, ilipata taarifa kuwa baadhi ya
wananchi wamemilikishwa viwanja hivyo bila kulipia gharama zilizohitajika kwa
mujibu wa taratibu zilizowekwa na Manispaa hiyo”.
“TAKUKURU imeweza kuwafikia baadhi ya
waliomilikishwa viwanja hivyo na kuwataka walipie gharama za mauzo ya viwanja
hivyo kama ilivyopaswa au viwanja husika vitangazwe upya ili kupata wanunuzi
watakaoweza kulipia gharama husika”.
“Wamiliki
waliofikiwa walikubali kufanya malipo ya viwanja hivyo kama walivyopaswa. Mpaka
sasa jumla ya TZS. 137,800,000/= kati ya
TZS. 800,000,000/= zimelipwa kwa
Manispaa ya Kahama kupitia Account ya Miscellaneous Deposit”.
“Aidha
TAKUKURU inaendelea kusimamia ulipwaji wa fedha zote zilizobaki ambazo ni
takriban TZS. 662,200,000/= ili
kuhakikisha viwanja vyote vinalipiwa na fedha zake zinaingia Serikalini”.amesema
Kessy
Katika kipindi hicho, TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga pia
imefuatilia miradi 10 ya sekta ya elimu yenye thamani ya shilingi bilioni 3.1
katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Kishapu na Manispaa ya Shinyanga.
Aidha, kupitia dawati la uchunguzi, taasisi hiyo
imepokea malalamiko 38, ambapo 20 kati yake yanahusiana na rushwa na uchunguzi
wake unaendelea, huku malalamiko 18 yakiwa hayahusiani na rushwa.