" TEA YATAJA MAFANIKIO YAKE MIAKA MINNE YA SERIKALI YA AWAMU YA SITA

TEA YATAJA MAFANIKIO YAKE MIAKA MINNE YA SERIKALI YA AWAMU YA SITA

Miradi ya Elimu 3,768 yatekelezwa, Bil 49.5 zatumika

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Dkt. Erasmus F. Kipesha, leo tarehe 25 Februari 2025, amezungumza na vyombo vya habari kuhusu mafanikio na mipango ya TEA katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Ameeleza kuwa TEA imefanikiwa kutekeleza miradi 3,768 yenye thamani ya Sh. Bilioni 49.5 katika kipindi hicho.

Katika mkutano huo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Idara ya Habari -MAELEZO, Dkt. Kipesha amesema katika kipindi hicho, TEA imefadhili ujenzi wa vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo, miundombinu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, nyumba za walimu, mabweni, maabara za sayansi, na majengo ya utawala.

Katika mwaka wa fedha 2024/2025, TEA, kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa inaousimamia, imepanga kutekeleza miradi 113 yenye thamani ya Sh. Bil 11.3, ambayo itanufaisha wanafunzi 29,482.

Miradi itakayofadhiliwa katika mwaka wa fedha 2024/2025 inajumuisha: ujenzi wa vyumba vya madarasa 45, ukarabati wa vyumba vya madarasa 11, ujenzi wa matundu ya vyoo 336, ujenzi wa nyumba za walimu 12, ujenzi wa mabweni 8 na ununzi wa vifaa vya TEHAMA kwa ajili ya shule 9

Aidha, kiasi cha Sh. Bilioni 3.0 kitatumika kuimarisha miundombinu ya utoaji wa mafunzo ya amali, ikiwa ni sehemu ya kuwezesha utekelezaji wa mtaala mpya wa elimu nchini.

Kuhusu michango kutoka kwa wadau, Mamlaka imepokea michango yenye thamani ya Sh. Bilioni 4.11 katika kipindi cha miaka minne, kuanzia mwaka 2021/2022 hadi 2024/2025, pamoja na vifaa vyenye thamani ya Shilingi milioni 269.3.

Post a Comment

Previous Post Next Post