" TEKNOLOJIA ZA KILIMO KUONGEZA UZALISHAJI WA PAMBA KISHAPU

TEKNOLOJIA ZA KILIMO KUONGEZA UZALISHAJI WA PAMBA KISHAPU

TEKNOLOJIA za Kilimo cha Pamba zinazosambazwa na Serikali kupitia Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), zimelenga kuongeza tija ya uzalishaji wa Pamba ili wakulima waweze kujikwamua kiuchumi na Taifa liongeze kipato kupitia fedha za kigeni.

Aidha, Teknolojia hizo ikiwemo matumizi ya ndege nyuki (drones), maboza na majembe kupalilia Pamba, zimerahisisha shughuli za kilimo ikiwemo Upandaji, Upaliliaji na Unyunyiziaji.

Akizungumza na waandishi wa Habari za Pamba, Mkaguzi wa Pamba wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga, Thadeo Mihayo amesema wilaya hiyo imepatiwa Ndege zisizo na rubani saba kwa ajili ya kunyunyizia mashamba ya Pamba na kwamba zitawafikia wakulima 30,000 katika msimu wa kilimo 2024/2025.

Amesema Wilaya ya Kishapu, ni moja kati ya wilaya nane za kimkakati zilizotengwa na serikali kwa ajili ya kuongeza tija ya uzalishaji wa Pamba na kwamba wamepatiwa ekapaki (chupa) za dawa 540,000.

 "Kutokana na Teknolojia mbalimbali zilizoletwa na serikali kupitia Bodi ya Pamba Tanzania, tunaamini uzalishaji utaongezeka kutoka kilo 250 kwa ekari moja na kufikia kilo 800 hadi 1200 kwa ekari moja" amesema.

Amesema serikali imeweka Mikakati ya kuongeza uzalishaji ikiwemo kusambaza Kamba ya kupandia na kufundisha wakulima kupanda kisasa kwa kutumia vipimo vya sentimita 60 kwa 30 tofauti na vipimo vya awali vya 90 kwa 40 na matumizi ya ndege zisizo na rubani badala ya kubeba pambu mgongoni.

"viuatilifu vimeletwa kwa wakati ili kudhibiti wadudu wanaoshambulia Pamba,
Mwaka jana tulikuwa na ndege nyuki wawili leo wako saba, Maafisa Kilimo kupitia BBT wamepelekwa hadi vijijini ili kuhudumia wakulima kila siku na kila kijiji kuna Afisa Kilimo wa Kijiji, ambaye anampa Elimu mkulima moja kwa moja." Mihayo.

Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wilaya ya Kishapu, Richard Manguwa ameishukuru serikali kuwekeza katika Uzalishaji wa Pamba ambapo zao hilo huchangia asilimia 50 ya Mapato kwenye Halmashauri yao.

Amesema katika msimu wa 2025/2026 wanatarajia kupata mavuno mengi ya Pamba kutokana na jitihada za Uwekezaji ikiwemo matumizi ya Teknolojia ya ndege nyuki pamoja na upatikanaji wa Maafisa Kilimo wa BBT vijijini.

"Zaidi ya asilimia 50 ya Mapato kwenye Halmashauri ya wilaya ya Kishapu hutegemea zao la Pamba, tunatarajia kupata mavuno mengi kutokana na Uwekezaji Mkubwa uliofanywa na serikali kwenye zao hili" amesema.

Mabula Mhalala, mkulima kutoka Kijiji cha Mwanulu wilaya ya Kishapu ameishukuru serikali kwa kuwasogezea huduma za Ugani katika vijiji vyao kwani wanatatuliwa changamoto zao kwa haraka.

Mwisho.



Post a Comment

Previous Post Next Post