" MASHINE TATU ZA KUSAGA ZAUNGUA MOTO KISHAPU MKOANI SHINYANGA MAHINDI, MPUNGA NA VIFAA VYOTE VYATEKETEA

MASHINE TATU ZA KUSAGA ZAUNGUA MOTO KISHAPU MKOANI SHINYANGA MAHINDI, MPUNGA NA VIFAA VYOTE VYATEKETEA

TAZAMA VIDEO

Na Mapuli Kitina Misalaba

Mashine ya kusaga unga inayomilikiwa na Mzee Joseph Pombe katika Kijiji cha Ipeja, Kata ya Itilima, Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, imeungua moto na kuteketeza kila kitu kilichokuwemo ndani baada ya hitilafu ya umeme.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ipeja, Jackson Mwabila, amesema tukio hilo limetokea Februari 24, 2025, ambapo moto huo ulianza ghafla na kusababisha hasara kubwa.

“Tarehe 24, 2, 2025 lilitokea tukio kwenye kijiji changu, kuna mashine ya kusaga unga ilitokea hitilafu ya umeme, moto ukalipuka na kuwasha nyumba yote. Yaani mpaka sasa ninavyoongea, nyumba imeteketea kabisa,” amesema Mwabila.

Ameeleza kuwa mashine tatu zilikuwepo ndani ya jengo hilo, ikiwemo mashine ya kusagia unga, mashine ya kukoboa mahindi na mashine ya kukoboa mpunga, lakini vyote vimeteketea kwa moto huo.

“Jitihada za kuuzima moto zilifanyika, tuliwapigia simu lakini waliwasili kwa kuchelewa. Walifanikiwa kuuzima moto huo lakini vifaa vyote vilikuwa tayari vimeteketea,” ameongeza Mwenyekiti huyo.

Pamoja na mashine hizo, ndani ya jengo kulikuwa na mahindi ya kusaga, mpunga, na bidhaa nyingine mbalimbali ambazo zote zimeangamia kutokana na moto huo.

Hadi sasa, tathmini ya hasara bado inaendelea kufanyika huku wananchi wakihimizwa kuchukua tahadhari dhidi ya majanga ya moto yanayoweza kuzuilika.















Post a Comment

Previous Post Next Post