Na Elisha Petro, Misalaba Media
Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Chama cha Mapinduzi
CCM Kata ya Ndembezi wakiongozwa na Mwenyekiti wa Umoja huo Linah Kazimiri
wametembelea kituo cha watoto yatima Bushushu Manispaa ya Shinyanga na kutoa
msaada wa vitu mbalimbali ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 48 ya
kuanzishwa kwa Chama cha Mapinduzi CCM.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo
Mwenyekiti Linah Kazimiri amewasisitiza Wajumbe wa umoja huo na jamii Kwa
ujumla kujifunza kupitia kituo hicho cha watoto yatima Bushushu ili kuendelea
kuwa na moyo wa majitoleo na kusaidia watu wenye uhitaji katika jamii.
"Ndugu
zangu kwanza niwapongeze kwa utayari wa kufika hapa na moyo wenu wa majitoleo
kuwasaidia watoto wetu lakini nimewaleta hapa ili tujifunze na jamii ijifunze
kupitia sisi juu ya umuhimu wa kuguswa kusaidia makundi yenye uhitaji katika
jamii zetu ikiwemo kituo hiki cha kulea watoto yatima na Kila mmoja wetu atoke
hapa akijua kuwa pale unapopata kile ulichojaliwa nacho basi kumbuka kusaidia
wahitaji isiishie leo tu bali iwe mwendelezo kila mara"
Awali akizungumza kabla ya kukabidhi vitu hivyo
Katibu wa UWT Kata ya Ndembezi Bi. Christina Stanslaus Milenge ameushukuru
uongozi wa kituo hicho kwa ushirikiano waliouonyesha na kuahidi kuwa
wataendelea kushirikiana na kutenga muda wao kufika kituoni hapo ili kuwa
karibu zaidi na watoto.
"Mama
yetu mpendwa na mlezi wa Kituo hiki kwanza kabisa nimefarijika kwa mapokezi
yenu makubwa na utayari wenu wa kutukaribisha kituoni hapa sisi UWT Kata ya
Ndembezi tumefika hapa kukaa na watoto wetu lakini pia tumewaletea ridhiki hii
ya vitu mbalimbali (Mchele,Vinywaji,Sabuni ) tunaomba muipokee lakini pia
tunaahidi kuendelea kushirikiana na kutenga muda wetu kufika mahali hapa ili kuwafariji
watoto wetu na kuwa karibu nao"
Kwa upande wake mmiliki wa Kituo cha kulelea watoto
yatima Bushushu Bi. Ayam Ally Said maarufu kwa jina la Mama yatima amewapongeza
viongozi na Wajumbe wa UWT Kata ya Ndembezi kwa msaada walioutoa na kutenga
muda wao kwenda kuwafariji watoto hao na kuwaomba waendelee kuwa na Umoja
,Upendo na Mshikamano kwa lengo la kusaidia makundi yote yenye uhitaji katika
jamii.
"Kwanza
kabisa niwashukuru kwa Umoja wenu kwa msaada huu mkubwa lakini pia kufika
katika kituo chetu na kuwasalimia watoto wenu naamini Mwenyezi Mungu
atawazidishia mlipogusa lakini niwaombe sana mwendelee kudumisha Umoja huu
mpendane na kuvumiliana katika kila hali najua sisi wakina mama tunanafasi
kubwa katika malezi ya watoto hawa niwaombe isiishie tu leo kwa sababu ni
maadhimisho ya CCM sisi milango yetu ipo wazi kila wakati mje kuwasalimia
watoto hawa sio lazima uje na kitu cha kushikika hata neno lako ni faraja tosha
naomba sana msirudi nyuma muendelee na Umoja huu"
Wakizungumza na Misalaba Media baadhi ya watoto
katika kituo hicho wameshukuru kwa msaada waliopokea kutoka UWT Kata ya
Ndembezi na kufanya Dua ya kushukuru na kuwaombea wote walioguswa na kutoa
msaada huo huku wakiwaomba waendelee kuwa na moyo wa majitoleo.
Hafla hiyo imetanguliwa na zoezi la upandaji wa miti ambapo viongozi mbalimbali wa Chama cha Mapinduzi CCM Kata ya Ndembezi wamehudhuria mwanzo hadi mwisho wa zoezi hilo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 48 ya kuanzishwa kwa Chama cha Mapinduzi CCM ambapo kilele chake ni tarehe 05.2.2025