UWT SHINYANGA YAADHIMISHA MIAKA 48 YA CCM KWA MATENDO YA HURUMA NA UPANDAJI MITI

Na Mapuli Kitina Misalaba

Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) Mkoa wa Shinyanga umeadhimisha miaka 48 ya CCM kwa kufanya matendo ya huruma, ikiwemo kutoa msaada kwa wagonjwa hospitalini na katika kituo cha afya, pamoja na kupanda miti ili kuunga mkono juhudi za serikali katika utunzaji wa mazingira.

Sherehe hizo kwa ngazi ya Mkoa zimefanyika katika Wilaya ya Shinyanga Vijijini Februari 1, 2025 ambapo wanachama na viongozi wa UWT wameshiriki zoezi la upandaji miti katika eneo la nyumba ya Katibu wa UWT wilayani humo.

Aidha, jumuiya hiyo imetoa msaada wa sabuni za unga na vipande, mafuta ya kujipaka, pamoja na juisi kwa wagonjwa waliolazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Shinyanga Vijijini, wakiwemo walioko katika wodi ya wazazi.

Katika hatua nyingine, UWT pia imetoa msaada wa mashuka kwa wagonjwa katika kituo cha Afya Nindo, ambapo msaada huo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 48 tangu kuanzishwa kwa CCM.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Shinyanga, Bi. Grace Samweli Bizuru, amesema kuwa wanawake wa UWT wanajivunia kuwa sehemu ya CCM kwa sababu chama hicho kinaendelea kuleta maendeleo chanya kila wakati.

Amewahimiza wananchi kuendelea kukiunga mkono chama hicho pamoja na viongozi wa serikali katika utekelezaji wa Ilani ya CCM ili kero na changamoto zinazowakabili wananchi ziweze kutatuliwa kwa ufanisi.

Aidha, Bi. Bizuru amesisitiza kuwa UWT Mkoa wa Shinyanga inaunga mkono uamuzi wa Mkutano Mkuu wa CCM wa kumpitisha Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo amebainisha kuwa jumuiya hiyo itaendelea kusimama bega kwa bega na Rais Samia kuhakikisha anapata ushindi mkubwa katika uchaguzi ujao.

Katika hotuba yake, Bi. Bizuru pia amewahimiza wanawake kuimarisha malezi bora kwa watoto wao ili waweze kukua katika misingi ya maadili mema huku akitoa wito kwa wanawake kupaza sauti dhidi ya vitendo vya ukatili vinavyowakumba wanawake na watoto ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa wahusika.

Kwa upande wake, Mgeni mwalikwa katika maadhimisho hayo, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Kahama na Mjumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Shinyanga, Simon Makoye Mayengo, ameipongeza Serikali ya awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM.

“Chama cha Mapinduzi kinafanya kazi kubwa chini ya Rais Samia Suluhu Hassan. Katika Mkoa wetu wa Shinyanga, tumeshuhudia ongezeko kubwa la miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa barabara za lami, madaraja, vituo vya afya na miundombinu mingine muhimu. Hatuna sababu ya kushindwa kumpa kura nyingi Rais wetu Samia Suluhu Hassan ili aendelee kutuletea maendeleo,” amesema Mayengo.

Amemalizia kwa kuwasihi wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi wakati wa uchaguzi ili kumpa ushindi wa kishindo Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Maadhimisho hayo yameacha alama ya upendo na mshikamano miongoni mwa wanajumuiya wa UWT na jamii kwa ujumla, huku yakionyesha dhamira ya CCM katika kuboresha maisha ya wananchi na kulinda mazingira kwa vizazi vijavyo.

 

 


Previous Post Next Post