" WAKULIMA 70,000 KUFIKIWA NA NDEGE NYUKI- IGUNGA

WAKULIMA 70,000 KUFIKIWA NA NDEGE NYUKI- IGUNGA

WAKULIMA zaidi ya 70,000 katika wilaya ya Igunga Mkoani Tabora wanatarajia kufikiwa na huduma ya unyunyiziaji wa mashamba yao bure kwa kutumia ndege zisizo na rubani (Drone) zilizotolewa na serikali kupitia Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) kwa lengo la kurahisisha zoezi hilo.


Teknolojia hiyo imeletwa na serikali ikiwa ni moja ya Mikakati yenye lengo la kuongeza uzalishaji wa Pamba ambapo itarahishisha upuliziaji ili kudhibiti wadudu wanaoshambulia zao hilo kwa wakati.

Akizungumza na Waandishi wa Habari za Pamba, waliotembelea mashamba kwa lengo la kujionea ufanisi wa Teknolojia hiyo, Mkaguzi wa Pamba wilayani Igunga, Benjamini Madama amesema kuwa katika wilaya hiyo wamepatiwa ndege nyuki saba ambazo zitawafikia wakulima zaidi ya 70,000.

Amesema Teknolojia hiyo imerahisisha zoezi la upuliziaji kwani awali wakulima walikuwa wanatumia pampu za kubeba mgongoni (Matabhi) ambapo zilikuwa zinawachosha na kukosa ufanisi.

"Hii Teknolojia inatumia dakika 10 kwa ekari moja, tofauti na pampu za mgongoni ambazo walitumia saa 1 kwa ekari moja...huduma hii ni bure na utasaidia Malengo ya kuongeza uzalishaji na tija ya zao la Pamba" amesema.

Ameeleza kuwa ndege nyuki wanagusa majani ya Pamba juu na chini kupitia upepo na kusambaza dawa kwenye mmea wa pamba na kwamba inatumia muda mfupi kunyunyizia eneo kubwa.

Ameongeza kuwa, Teknolojia hiyo inapunguza gharama kwa wakulima na pia itahudumia wakulima wasiochanganya mazao na waliokata masalia ya Pamba.

Kwa upande wao wakulima wa pamba wamesema kuwa awali walikuwa wanatumia pampu za kubeba mgongoni ambazo zilikuwa zinawasababishia maumivu pamoja na kuchukua muda mrefu kupulizia mashamba.

Robart Masanja, mkulima wa Pamba Kijiji cha Mbutu wilayani Igunga, amesema Teknolojia hiyo imerahisisha shughuli ya upuliziaji kwa wakulima wenye mashamba makubwa waliokuwa wanatumia muda mrefu kupulizia.

Juma Nkwabi, mkulima wa Kijiji cha Mwabakima wilayani Igunga, amesema Teknolojia hiyo imekuja kwa muda mwafaka ili kurahisisha shughuli za upuliziaji wa sumu kwenye zao la Pamba.





Post a Comment

Previous Post Next Post