Na Mapuli Kitina Misalaba
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Anamringa Macha,
ameongoza uzinduzi wa kampeni maalum ya kuibua na kuwafikia wananchi wenye
vimelea vya ugonjwa wa kifua kikuu (TB) ambao bado hawajafikiwa na huduma za
uchunguzi na matibabu.
Kampeni hiyo inafanyika bure kwa wananchi wote,
ikiwa na lengo la kutokomeza mzunguko wa maambukizi ya TB katika jamii ya
Shinyanga.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Yudas
Ndungile, amesema kampeni hiyo inalenga kufanikisha upimaji wa watu takribani
1,349, idadi inayokadiriwa kuwa na maambukizi kwa mujibu wa takwimu za
viashiria vya ugonjwa huo.
"Hii
ni kampeni harakishi ya kuibua na kuwafikia wananchi wote wenye vimelea vya
kifua kikuu na ambao hawajawahi kufikiwa. Kampeni hii itakuwa bure, wananchi
wanakaribishwa kupima, na wale watakaogundulika na ugonjwa watapatiwa matibabu
bure. Lengo letu ni kuhakikisha hakuna mzunguko wa maambukizi ya kifua kikuu
katika jamii ya Mkoa wa Shinyanga," amesema Dkt. Ndungile.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya
Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya ndani,
Dkt. Luzila John, ameeleza kuhusu ugonjwa wa kifua kikuu, akibainisha kuwa ni
maradhi yanayoambukizwa kwa njia ya hewa na yamesababisha vifo vya watu milioni
2.5 kwa mwaka 2023 duniani, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).
"Tafiti
zinaonesha kuwa asilimia 25 ya watu tayari wana maambukizi ya wadudu wa TB,
ingawa si wote wanaougua mara moja. Dalili kuu za ugonjwa huu ni kikohozi cha
muda mrefu, homa za mara kwa mara, kupungua uzito, kutoka jasho usiku na dalili
nyingine zinazotegemea sehemu iliyoathirika mwilini,"
amesema Dkt. Luzila.
Baadhi ya wananchi waliojitokeza kwenye uzinduzi huo
wameeleza kufurahishwa na huduma hiyo kutolewa bure, huku wakiwataka wataalamu
wa afya kuhakikisha kuwa inawafikia wananchi wengi kwa ubora unaotakiwa.
Uzinduzi huo umefanyika katika Hospitali ya Rufaa ya
Mkoa wa Shinyanga Mwawaza, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo
Waganga Wakuu wa Halmashauri zote sita za Shinyanga, Wakurugenzi wa
Halmashauri, viongozi wa dini, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga Mhe.
Elias Ramadhan Masumbuko, pamoja na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mhe.
Anord Makombe.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Anamringa Macha
akizindua kampeni maalum ya kuibua na kuwafikia wananchi wenye vimelea vya
ugonjwa wa kifua kikuu (TB) katika Mkoa wa Shinyanga.
Post a Comment