Na Mapuli Kitina Misalaba
Kampeni harakishi ya upimaji wa ugonjwa wa kifua
kikuu (TB) inaendelea mkoani Shinyanga, ambapo hadi kufikia Februari 10, 2025,
wagonjwa 464 wamebainika kati ya lengo la wagonjwa 1,349.
Akizungumza na Misalaba Media, Mratibu wa Kifua Kikuu
na Ukoma Mkoa wa Shinyanga Dkt. Laurent Mhembe, amesema kampeni hiyo inahusisha
Halmashauri zote sita za Mkoa huo, ambapo jumla ya vituo 72 vimeshiriki
kikamilifu.
"Katika
zoezi hili, kila Halmashauri tumetambua vituo 12, hivyo tumekuwa na vituo 72
vinavyotoa huduma kila kituo kilikuwa na wahudumu wa afya wawili, hivyo jumla
ya wahudumu 144 wa ngazi ya jamii walihusika katika kampeni hii,"
amesema Dkt. Mhembe.
Kwa mujibu wa Dkt. Mhembe, takwimu za mwaka jana
zilionyesha kuwa baadhi ya Halmashauri hazikufikia malengo ya kubaini idadi ya
wagonjwa waliotarajiwa. Hali hiyo ilikuwa kama ifuatavyo:
Halmashauri
ya Kahama - upungufu wa wagonjwa 143
Halmashauri
ya Kishapu - upungufu wa wagonjwa 140
Halmashauri
ya Msalala - upungufu wa wagonjwa 241
Shinyanga
Vijijini - upungufu wa wagonjwa 205
Halmashauri
ya Manispaa ya Shinyanga - upungufu wa wagonjwa
490
Halmashauri
ya Ushetu - upungufu wa wagonjwa 130
Hali hiyo ilisababisha upungufu wa wagonjwa 1,049
kutambuliwa mwaka jana, hivyo kuhitaji juhudi za ziada mwaka huu na kwamba kampeni
inayoendelea sasa, jumla ya watu zaidi ya 8,000 tayari wamepimwa, na wagonjwa
464 wamebainika na kuanza kutumia dawa.
Baadhi ya wananchi waliojitokeza kupima wameishukuru
serikali kwa kutoa huduma hiyo bure, huku wakiwataka wenzao kujitokeza kwa
wingi ili kupata vipimo na matibabu kwa wakati.
Kampeni hii inaendelea mkoani Shinyanga kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu ugonjwa wa kifua kikuu na kuhakikisha wagonjwa wanapatikana mapema ili kupata matibabu stahiki.
Post a Comment