Mkuu wa chuo cha ufundi stadi Veta Mwakata Kahama (St Fransis Vacation Center) Father John akipokea zawadi kutoka kwa wahitimu wa mahafali ya 25 ya chuo hicho.
Shirika la Wanawake katika sheria na Maendeleo Barani Afrika(WilDAF) kwa kushirikiana na UN-FPA kwa ufadhili wa serikali ya Finland, kupitia mradi wa ‘Chaguo langu haki yangu’ limefanikiwa kuwaokoa mabinti balehe na vijana wamama zaidi ya 700 kutokana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Afisa mradi wa mradi wa chaguo langu haki yangu Joyce Kessy katika mikoa ya Mara na Shinyanga amesema mradi huo unalenga kuwafikia mabinti balehe na wanawake vijana kati ya umri wa miaka 10-19 na 15 – 24, kuwalinda dhidi ya ukatili, ndoa na mimba za utotoni pamoja na ukeketaji kwa mkoa wa Mara.
Ameyazungumza hayo muda mfupi baada ya kumalizika kwa mahafali ya 25 ya chuo cha ufundi stadi Veta Mwakata Kahama (St Fransis Vacation Center) yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, ambapo mabinti balehe na wanawake vijana zaidi ya 270 wamehitimu na kutunukiwa vyeti vyao tayari kwa kujiajiri/kuajiriwa.
Bi Kessy amesema mradi huo pia umelenga zaidi wenye ulemavu katika makundi hayo kwani wanaonekana kusahaulika zaidi na jamii, huku likiwa katika uhatarishi mkubwa wa vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia.
Amesema WiLDAF kwa kushirikiana na shirika la kimataifa la idadi ya watu ulimwenguni UNFPA kwa ufadhili wa serikali ya Finland, iliona suala kubwa ni kutoa nafasi kwa wale waliopo nje ya shule kujiunga na vyo vya VETA ikiwemo VTC Mwakata ili kujifunza fani tofauti tofauti ili wawe na uwezo wa kujiajiri, kuajiriwa ili kujikwamua kiuchumi hali itakayowasaidia kuepukana na vitendo vya ukatili.
“Kama tunavyofahamu kwamba uchumi duni unachangia kwa kiasi kikubwa sana vitendo vya ukatili, kwa hiyo sisi tunamwezesha binti kiuchumi, tunampa ujuzi, ili aweze kuinuka kiuchumi kama nyenzo ya kujikwamua dhidi ya vitendo vya ukatili” Alisema Kessy
Amesema wahitimu hao baada ya mafunzo wanawapatia vifaa kulingana na fani walizosomea ili waweze kutekeleza ujuzi wao kwa vitendo na kubadilisha maisha yao, na kwamba mabinti hao 787 wamefikiwa katika kipindi cha miaka mitatu ya utekelezaji wa mradi wa “Chaguo langu, haki yangu” uliotekelezwa katika wilaya mbili za mkoa wa Mara(Butiama na Tarime) na mbili za mkoa wa Shinyanga (Kishapu na Kahama).
Kati ya mabinti hao 263 wameshapatiwa vifaa na kwamba waliobaki wanakwenda kupatiwa vifaa vyao hivi karibuni kulingana na fani husika baada ya awamu hii ya mwisho kuhitimu, na kueleza kuwa mambo haya yote yanafanyika kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania.
Akizungumza kwa niaba ya serikali ya manispaa ya Kahama, wakati wa mahafali hayo, afisa ustawi wa jamii kutoka manispaa hiyo Swahiba Chemchem alisema kuwa, serikali iko tayari kuwaunga mkono mabinti hao hata wanaporejea mtaani, sambamba na kuwaunganisha na fursa mbalimbali zitakazojitokeza.
Baadhi ya wahitimu Vaileth Charles mhitimu wa fani ya ushonaji kutoka Kishapu, aliishukuru WiLDAF kwa kuwawezesha kutimiza ndoto zao na kuwaomba waongeze muda zaidi wa utekelezaji wa mradi huo kwa mabinti wengi bad oni wahanga wa ukatili haswa mimba na ndoa za utotoni, sambamba na wao kutokuwa tegemezi.
Awali akisoma risala ya wahitimu kwa niaba ya wahitimu wenzake, kwa mgeni rasmi, ambaye ni afisa mahusiano wa kampuni ya uchimbaji wa madini ya dhahabu – Canuck Clarence Haule, mhitimu Debora Martin amelishukuru shirika la WiLDAF, uongozi wa chuo pamoja na serikali kwa kuwapatia fursa hiyo, ambayo imewasaidia kupata ujuzi mbalimbali, utakaowasaidia kujiajiri au kuajiriwa, huku wakiomba zinapotokea fursa mgodini hapo basi viongozi wasisite kuwapa kipaumbele.
Kwa upande wake Mwalimu wa chuo cha ufundi stadi Veta Mwakata Kahama (St Fransis Vacation Center) Mwalimu Monica Daniel akisoma historia ya chuo hicho alisema kimeanzishwa mwaka 2003, na kilianzishwa na padreJoseph Elian aliyekuwa mkuu wa chuo chini ya mkuu wa shirika la Mt Fransisco wa sales.
Mwalimu Monica alisema chuo kimefanikiwa kuwajengea uwezo mzuri wanafunzi wao ikiwemo tabia njema za kiroho na kuishi katika hofu ya Mungu, lakini pia chuo kimefanikiwa kuwatafutia wanafunzi wao maeneo ya kujifunza kwa vitendo baada ya kuhitimu mafunzo yao.
Akizungumza kwenye mahafali hayo, mgeni rasmi ambaye ni afisa mahusiano wa kampuni ya uchimbaji wa madini ya dhahabu ya Canuck iliyopo kata ya Mwakata Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga Clarence Haule, kwa niaba ya meneja mkuu wa kampuni hiyo ameahidi kuchangia mifuko 50 ya saruji, kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa uzio wa chuo hicho, ikiwa ni utekelezaji kwa vitendo dhima ya kurejesha sehemu ya faida yake kwenye jamii inayozunguka mgodi (CSR).
Haule amesema uwepo wa uzio chuoni hapo, utasaidia usalama kwa wanafunzi, mali za chuo na kuondoa migogoro itokanayo na mwingiliano kati ya wanakijiji na chuo, huku akiutaka uongozi wa chuo kuainisha aina za mashine na gharama zake ili mgodi uone namna ya kusaidia kufanikisha jambo hilo.
Akizungumzia changamoto ya maji inayokikabili chuo hicho pamoja na maeneo jirani, Haule amesema tayari mgodi umeanza mchakato wa kupata maji safi na salama kutoka ziwa Victoria, na chuo hicho ni miongoni mwa maeneo yatakayonufaika zaidi na ujio wa maji hayo, na kwamba yameshafikishwa kwenye mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Kahama – KUWASA, na sasa wanasubiri utekelezaji wao.
“Tunatambua kuwa hapa kijijini swala la upatikanaji wa maji safi na salama kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi na jamii na jamii bado ni tatizo, hivyo kampuni inawaomba wote kwa ujumla tuwe na subra kwa maana kampuni imekwishafikisha ombi la kufikishiwa huduma na KUWASA” Alisema Haule
Baadhi ya wanafunzi na wahitimu wa chuo cha ufundi stadi Veta Mwakata Kahama (St Fransis Vacation Center), wakitoa burudani, wakati wa mahafali ya 25 ya chuo hicho

Mkuu wa chuo cha ufundi stadi Veta Mwakata , Father John akizungumza wakati wa mahafali ya 25 ya chuo hicho.

Mgeni rasmi katika mahafali ya 25 ya chuo cha ufundi stadi Veta Mwakata Kahama (St Francis Vacation Center) ambaye ni afisa mahusiano wa kampuni ya uchimbaji wa madini ya dhahabu ya Canuck iliyopo kata ya Mwakata Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga Clarence Haule kushoto, akiwa na mmoja wa wazazi wa wahitimu, wakiwatunza watumbuizaji.

mkurugenzi wa WiLDAF akizungumza na wahitimu pamoja na wazazi kwenye mahafali ya 25 ya chuo cha ufundi stadi Veta Mwakata

Wahitimu wa fani ya umeme katika chuo cha ufundi stadi Veta Mwakata Kahama (St Francis Vacation Center) wakionyesha kwa vitendo kile walichojifunza wakati wa mahafali ya 25 ya chuo hicho mbele ya mgeni rasmi ambaye ni afisa mahusiano wa kampuni ya uchimbaji wa madini ya dhahabu ya Canuck iliyopo kata ya Mwakata Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga Clarence Haule.

Mgeni rasmi katika mahafali ya 25 ya chuo cha ufundi stadi Veta Mwakata Kahama (St Francis Vacation Center) ambaye ni afisa mahusiano wa kampuni ya uchimbaji wa madini ya dhahabu ya Canuck iliyopo kata ya Mwakata Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga Clarence Haule kulia akitoa vyeti kwa wahitimu.

Matron wa chuo cha ufundi stadi Veta Mwakata Kahama (St Francia Vacation Center) Magreth Alimosa, akiongoza zoezi la ukataji wa keki ya mahafali ya 25 ya VTC Mwakata kwa wahitimu na wageni waalikwa.
Post a Comment