Mwanamke anayefahamika kwa jina la Anna Masele,
anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 70, amekutwa amefariki dunia ndani ya
chumba chake asubuhi ya leo katika Mtaa wa Dome, Kata ya Ndembezi, Manispaa ya
Shinyanga.
Taarifa za tukio hilo
zimetolewa na Mwenyekiti wa mtaa huo, Solomon Nalinga Najulwa maarufu kama
Cheupe, wakati akizungumza na Misalaba Media ambaye amesema alipokea simu
kutoka kwa msamaria mwema aliyetoa taarifa kuhusu kifo hicho leo Machi 8, 2025.
Kwa mujibu wa wajukuu wa marehemu, usiku wa kuamkia
leo walikula chakula cha pamoja na bibi yao, ambaye hakuwa na tatizo lolote la
kiafya. Baada ya chakula, kila mmoja alielekea kulala, huku marehemu akifunga
mlango wa chumba chake kwa ndani kama kawaida.
“Nilipigiwa
simu na msamaria mwema akiniambia kuwa kuna bibi anayedhaniwa kuwa amefariki dunia
katika mtaa wangu. Nilichukua hatua ya kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kisha
nikaenda kwenye eneo la tukio na kujiridhisha kuwa kweli mama huyo alikuwa
amefariki akiwa ndani ya nyumba yake,” amesema Najulwa.
“Asubuhi walipoamka walimgongea mlango ili
amfungulie, lakini hakujibu. Walipoona hali si ya kawaida, walikubaliana
kubomoa sehemu ya mlango ili mmoja wao apite ndani, ndipo walipomkuta bibi yao
akiwa tayari amefariki dunia,” ameongeza Najulwa.
Jeshi la Polisi
lilifika eneo la tukio na baada ya kufanya uchunguzi wa awali, lilichukua mwili
wa marehemu na kuupeleka hospitalini kwa taratibu zaidi.
Mpaka sasa mwili wa Anna Masele upo mochwari huku
ndugu wakiendelea na maandalizi ya mazishi.
MISALABA MEDIA:
Tutaendelea kufuatilia taarifa zaidi kuhusu tukio hili.
Post a Comment