" CCM YAHAKIKISHA KUENDELEA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WANANCHI, WASIRA ATOA MAAGIZO KWA WACHIMBAJI WA MADINI KAHAMA

CCM YAHAKIKISHA KUENDELEA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WANANCHI, WASIRA ATOA MAAGIZO KWA WACHIMBAJI WA MADINI KAHAMA

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira, akizungumza kwenye mkutano wake wa hadhara uliofanyika wilayani Kahama leo Machi 27, 2025.

Na Mapuli Kitina Misalaba

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira, amesema kuwa chama hicho hakina mpango wa kuondoka madarakani kwa sababu kimeendelea kuwa nguzo ya amani na maendeleo ya Tanzania.

Wasira ametoa kauli hiyo leo Machi 27, 2025, wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani Kahama, ambapo ameeleza kuwa CCM kimekuwa kikitatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi, huku maendeleo makubwa yakishuhudiwa hasa katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

"CCM ni chama kilichounganisha vyama vilivyoleta ukombozi Tanzania na Afrika. Tumejenga umoja wa kitaifa kwa makabila yote, hatujawahi kupigana wenyewe kwa wenyewe, tunasuluhisha migogoro ya mataifa mengine na kupokea wakimbizi wakati nchi nyingine zinapigana. Vyama vidogo haviwezi kujilinganisha nasi. Hatutoki madarakani kwa sababu wananchi wanatuunga mkono na maendeleo yanaonekana," amesema Wasira.

Akizungumzia maendeleo yaliyofanikishwa na Rais Samia, Wasira amebainisha kuwa miradi mikubwa iliyoanzishwa na Hayati John Magufuli imeendelea kwa kasi kubwa chini ya uongozi wa Rais wa awamu ya sita.

"SGR iliyoanzishwa na Magufuli sasa imekamilika kwa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro, na inaendelea kujengwa hadi Mwanza kupitia Isaka, Kahama. Bwawa la umeme la Julius Nyerere lilikuwa asilimia 30 Magufuli alipofariki, sasa limefikia asilimia 70 na tayari tunaumeme wa mradi huo. Daraja la Busisi pia limeendelea kujengwa na sasa liko zaidi ya asilimia 60 ya utekelezaji wake," amesema Wasira.

Katika mkutano huo, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kutoka Mkoa wa Shinyanga, Gasper Kileo (GAKI), ameeleza kuwa Shinyanga itaendelea kuwa ngome ya CCM na kuhakikisha ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu wa 2025.

"Shinyanga tulikuwa nafasi ya pili kwa kura nyingi mwaka 2020, lakini 2025 tutakuwa wa kwanza. Rais wetu Dkt. Samia na mgombea mwenza wake Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi tutawapatia kura za kutosha," amesema Kileo.

Aidha, Wajumbe wengine wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa wamewataka wanachama wa CCM kuendelea kushikamana na kuwatumikia wananchi kwa kutatua changamoto mbalimbali za kijamii.

 Pia, wamelaani tukio la kudaiwa kushambuliwa kwa mwenezi wa Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA) Taifa, Bi. Sigrada Mligo, wakimtaka Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa kutoa tamko rasmi kuhusu tukio hilo.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mabala Mlolwa, ameeleza changamoto mbalimbali zinazowakabili wachimbaji wadogo wa madini wilayani Kahama, huku akiomba ziweze kushughulikiwa ambapo Wasira ametoa maagizo kwamba wachimbaji hao wasisumbuliwe na akaahidi kuwa changamoto zao zitatatuliwa.

Wakati huo huo, amebainisha kuwa changamoto za kodi kwa wafanyabiashara pia zitashughulikiwa.

Katika hatua nyingine, Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani, ameiomba Serikali kuongeza idadi ya mameneja wa TARURA ili kila Halmashauri katika Wilaya ya Kahama iwe na Menaja kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa miradi ya barabara.

Mkutano huo umehudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa chama na serikali, akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mhe. Mboni Mhita ambapo pamoja na mambo mengine Wasira amefungua shina la wajasiriamali katika Stendi ya CDT wilayani Kahama.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira, akizungumza kwenye mkutano wake wa hadhara uliofanyika wilayani Kahama leo Machi 27, 2025.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira, akizungumza kwenye mkutano wake wa hadhara uliofanyika wilayani Kahama leo Machi 27, 2025.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kutoka Mkoa wa Shinyanga, Gasper Kileo (GAKI), akizungumza kwenye mkutano huo wa hadhara Wilaya ya Kahama leo Machi 27, 2025.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mabala Mlolwa, akieleza changamoto za wachimbaji wadogo wa madini.

Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani, akizungumza kwenye mkutano huo wa hadhara Wilaya ya Kahama leo Machi 27, 2025.

Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani, akizungumza kwenye mkutano huo wa hadhara Wilaya ya Kahama leo Machi 27, 2025.

Awali Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira,akiwasili katika mkutano wa hadhara Wilaya ya kahama ambapo ameongeza na viongozi mbalimbali.







Post a Comment

Previous Post Next Post