" DKT. JANABI AHADHARISHA VIFO MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA

DKT. JANABI AHADHARISHA VIFO MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA

  


MKURUGENZI Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Profesa Mohamed Janabi amehimiza jamii kubadili mtindo wa maisha kuepuka vifo vinavyosababishwa na magonjwa yasiyoambukiza.

Profesa Janabi alisema hayo katika kipindi cha Busati la Mtoro kilichorushwa na kituo cha televisheni cha ZBC2 jana jioni.

Alisema ugonjwa wa moyo unaua watu milioni 18 duniani kila mwaka na shinikizo la damu la juu linaua watu milioni 9.4 kila mwaka duniani.

Profesa Janabi alisema ugonjwa wa shinikizo la damu umekuwa tishio nchini kwa sababu kila wanaume wanne mmoja wao ana shinikizo la juu la damu bila kujijua hali ambayo ni ya hatari.

Ameonya matumizi ya chumvi nyingi akisema kila mtu anatakiwa kula chakula chenye chumvi ambayo hawezi kuihisi mdomoni. Alisema kuwa chumvi ni kichocheo cha vifo vitokanavyo na shinikizo la juu la damu.

“Kuna watu wenye shinikizo la damu la juu lakini wao wenyewe hawajui kwa sababu hawana desturi ya kupima shinikizo la damu. Wapo wanaojua kuwa wana tatizo hilo lakini katika matumizi ya dawa hawatumii ipasavyo, mara leo katumia lakini kesho kaacha hali ambayo ni hatari sana,” alisema Profesa Janabi.

Aliongeza: “Ushauri wangu kwa wananchi, kila mwaka wajenge utaratibu wa kupima shinikizo la juu la damu ili kuokoa afya kwani taratibu linaua macho, linaua nguvu za kiume”.

Profesa Janabi alisema hakuna dalili mahususi inayoashiria kuwa na shinikizo la damu, hivyo wananchi wanatakiwa kutoishi kwa mazoea kuwa akihisi vinginevyo anajua ni shinikizo la damu.

Alisema ugonjwa wa kiharusi unaua watu milioni 6.5 kila mwaka duniani.

Profesa Janabi alisema kiharusi kinasababishwa na shinikizo la juu la damu na vipo vya aina mbili.

Kipo kiharusi kinachosababishwa na kupasuka kwa mshipa kichwani ambacho ndicho kibaya zaidi na aina ya pili ni kiharusi kinachosababishwa na kuminywa kwa mshipa unaopeleka damu kichwani.

Kuhusu ugonjwa wa saratani, alisema unaua watu milioni 9.6 kila mwaka duniani.

“Ugonjwa mwingine ni wa figo ambao umeathiri watu zaidi ya milioni 850 duniani. Ugonjwa mwingine ambao umekuja karibuni ni mpya ni afya ya akili ambao unaua watu milioni moja kila mwaka duniani,” alisema Profesa Janabi.

Pia, alisema watu zaidi ya milioni 2.5 wanafariki dunia kila mwaka kutokana na matatizo ya njia ya chakula kutoka mdomoni hadi kwenye haja kubwa.

Profesa Janabi alisema ajali za barabarani limekuwa tatizo lingine kwa kuwa kila mwaka watu milioni 1.3 wanapoteza maisha na zaidi ya milioni 50 wanapata ulemavu.

Alisema uvutaji wa sigara unaangamiza watu zaidi ya milioni saba duniani kila mwaka kutokana na kusababisha saratani na pumu. Aidha, watu milioni 1.2 wanaokaa karibu na wavuta sigara wanakufa kila mwaka.

Kwa upande wa kisukari, Profesa Janabi alisema ugonjwa huo upo wa aina mbili kwa maana ya aina ya kwanza ya kuzaliwa na aina ya pili inayosababishwa na mtindo wa maisha.

Post a Comment

Previous Post Next Post