MKURUGENZI Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Profesa Mohamed Janabi amehimiza jamii kubadili mtindo wa maisha kuepuka vifo vinavyosababishwa na magonjwa yasiyoambukiza.
Profesa Janabi
alisema hayo katika kipindi cha Busati la Mtoro kilichorushwa na kituo cha
televisheni cha ZBC2 jana jioni.
Alisema ugonjwa wa
moyo unaua watu milioni 18 duniani kila mwaka na shinikizo la damu la juu
linaua watu milioni 9.4 kila mwaka duniani.
Profesa Janabi
alisema ugonjwa wa shinikizo la damu umekuwa tishio nchini kwa sababu kila
wanaume wanne mmoja wao ana shinikizo la juu la damu bila kujijua hali ambayo
ni ya hatari.
Ameonya matumizi ya
chumvi nyingi akisema kila mtu anatakiwa kula chakula chenye chumvi ambayo
hawezi kuihisi mdomoni. Alisema kuwa chumvi ni kichocheo cha vifo vitokanavyo
na shinikizo la juu la damu.
“Kuna watu wenye
shinikizo la damu la juu lakini wao wenyewe hawajui kwa sababu hawana desturi
ya kupima shinikizo la damu. Wapo wanaojua kuwa wana tatizo hilo lakini katika
matumizi ya dawa hawatumii ipasavyo, mara leo katumia lakini kesho kaacha hali
ambayo ni hatari sana,” alisema Profesa Janabi.
Aliongeza: “Ushauri
wangu kwa wananchi, kila mwaka wajenge utaratibu wa kupima shinikizo la juu la
damu ili kuokoa afya kwani taratibu linaua macho, linaua nguvu za kiume”.
Profesa Janabi
alisema hakuna dalili mahususi inayoashiria kuwa na shinikizo la damu, hivyo
wananchi wanatakiwa kutoishi kwa mazoea kuwa akihisi vinginevyo anajua ni
shinikizo la damu.
Alisema ugonjwa wa
kiharusi unaua watu milioni 6.5 kila mwaka duniani.
Profesa Janabi
alisema kiharusi kinasababishwa na shinikizo la juu la damu na vipo vya aina
mbili.
Kipo kiharusi
kinachosababishwa na kupasuka kwa mshipa kichwani ambacho ndicho kibaya zaidi
na aina ya pili ni kiharusi kinachosababishwa na kuminywa kwa mshipa unaopeleka
damu kichwani.
Kuhusu ugonjwa wa
saratani, alisema unaua watu milioni 9.6 kila mwaka duniani.
“Ugonjwa mwingine ni
wa figo ambao umeathiri watu zaidi ya milioni 850 duniani. Ugonjwa mwingine
ambao umekuja karibuni ni mpya ni afya ya akili ambao unaua watu milioni moja
kila mwaka duniani,” alisema Profesa Janabi.
Pia, alisema watu
zaidi ya milioni 2.5 wanafariki dunia kila mwaka kutokana na matatizo ya njia
ya chakula kutoka mdomoni hadi kwenye haja kubwa.
Profesa Janabi
alisema ajali za barabarani limekuwa tatizo lingine kwa kuwa kila mwaka watu
milioni 1.3 wanapoteza maisha na zaidi ya milioni 50 wanapata ulemavu.
Alisema uvutaji wa
sigara unaangamiza watu zaidi ya milioni saba duniani kila mwaka kutokana na
kusababisha saratani na pumu. Aidha, watu milioni 1.2 wanaokaa karibu na wavuta
sigara wanakufa kila mwaka.
Kwa upande wa
kisukari, Profesa Janabi alisema ugonjwa huo upo wa aina mbili kwa maana ya
aina ya kwanza ya kuzaliwa na aina ya pili inayosababishwa na mtindo wa maisha.
Post a Comment