" DODOMA JIJI FC YATUA DAR KIBABE KUMINYANA NA SIMBA SC

DODOMA JIJI FC YATUA DAR KIBABE KUMINYANA NA SIMBA SC




Na Mussa Richard,

Klabu ya Soka ya Dodoma Jiji FC, itashuka dimbani hapo kesho kumenyana na klabu ya Soka ya Simba SC, katika mchezo wa ligi kuu ya NBC Tanzania bara, mchezo utakaopigwa katika dimba la KMC Complex Mwenge, Dar es salaam majira ya saa 10 kamili jioni.

Akizungumzia maandalizi ya timu, Kocha mkuu wa Dodoma Jiji FC, Mecky Mexime wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuelekea mchezo wa Simba SC, alisema “tunamshukuru Mungu tumefika Dar es Salaam salama, jana tumefanya mazoezi mepesi ya kuiweka miili sawa, tunajua mchezo utakuwa ni mgumu kwa pande zote, ukizingatia kwasasa ligi inaelekea ukingoni. Alama tatu kwa kila mchezo ni muhimu ili tuweze kifikia malengo yetu ya kumaliza ligi tukiwa nafasi za juu kwenye msimamo, maandalizi yote ya kucheza na Simba SC, tumeyafanya tukiwa Dodoma. Hapa tumekuja kukifanyia kazi kile tulichojifunza kwenye uwanja wa mazoezi’’.

Nae Abdi Banda, mchezaji wa Klabu ya Soka ya Dodoma Jiji FC, akawaita mashabiki wa Dodoma Jiji FC, waliopo Dar es Salaam na maeneo jirani, kufika kwa wingi uwanjani na kuwaunga mkono wachezaji pamoja na benchi la ufundi.

“Kwanza tunamshukuru Mungu tumefika kituo cha mchezo salama, kwa niaba ya wachezaji wenzangu tupo salama, na tayali kwaajili ya mchezo wa kesho. Niwaombe mashabiki wetu popote pale walipo waje kwa wingi uwanjani, kuna walio safari kutoka Dodoma kwaajili ya kuja kutuunga mkono. Sisi kama wachezaji tunafarijika sana na tunawaahidi kuwa tutapambana kuhakikisha tunapata alama katika mchezo wa kesho, lakini kwa wale ambao wamebaki nyumbani wasiache kutuombea ili tuweze kuibuka na ushindi kwenye mchezo wa kesho” alisema Banda.

Dodoma Jiji FC, imesafiri na jumla ya wachezaji 21, benchi la ufundi pamoja na viongozi ikiwa katika nafasi ya nane katika msimamo wa Ligi kuu ikijikusanyia alama 27, ikishuka dimbani mara 22.

Post a Comment

Previous Post Next Post