Kwa mara ya pili, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeshinda tena tuzo ya Uhusiano Mwema na Vyombo vya habari nchini, kwa mwaka 2024 ikidhihirisha namna taasisi hiyo inavyothamini ushirikano na uhuru wa vyombo vya habari katika kuuhabarisha umma kuhusu shughuli za udhibiti wa huduma za nishati na maji.
Tuzo hiyo iliyotolewa jana(29.3.2024) na Chama cha
Maofisa Uhusiano Tanzania (PRST), baada ya mchuano mkali uliohusisha taasisi
nyingi imeipa EWURA heshima na ari ya kuendelea kudumisha uhusiano wake thabiti
na vyombo vya habari pamoja na waandishi wa habari nchini.
Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa EWURA, Bw. Titus
Kaguo alisema ushindi huo kwa mara ya pili mfululizo ni kielelezo cha utawala
bora, uwazi, uwajibikaji, na miongozo inayotolewa na Bodi na Menejimenti ya
EWURA, chini ya mwemyekiti wake Prof. Mark Mwandosya na Mkurugenzi wake Mkuu,
Dkt. James Mwainyekule.
Vigezo vilivyotumika kuipatia EWURA ushindi huo ni
kuwa na mpango mkakati bora wa ushirikishwaji wa vyombo vya habari, ubora wa
maudhui na uthabiti wa utoaji taarifa pamoja na mtazamo walionao vyombo vya
habari kuhusu Mamlaka hiyo.
Wakati huo huo, Bi. Janeth Mesomampya, ambaye ni
Ofisa Uhusiano wa EWURA amepokea tuzo ya Ofisa Uhusiano bora kwa mwaka 2024,
akiwa mmoja wa washindi watano katika tuzo hizo.
Rais wa PRST Bw. Assah Mwambene, alisema utoaji wa
tuzo hizo ni chachu kwa wataalam walioko kwenye kada hiyo kufanya kazi zao kwa
ubora zaidi ili kuimarisha huduma katika maeneo yao ya utendaji.
EWURA ilipata tuzo ya aina hiyo pia kwa mwaka 2022,
iliyotolewa na PRST kutambua mchango wake katika kushirikiana vyema na vyombo
vya habari nchini.
Post a Comment