Mwanamke mmoja aitwaye Agatha Daniel Nyahuma mwenye
umri wa Miaka 32, mkazi wa kijiji cha Bugayambelele, amefariki dunia baada ya
kushambuliwa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali na mtu au watu wasiojulikana.
Akizungumza na Misalaba Media, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP
Kennedy Mgani, amesema tukio hilo limetokea mnamo Machi 9, 2025, majira ya saa
12 asubuhi katika mtaa wa Sido, eneo la Buhangija, kata ya Ibinzamata, Manispaa
ya Shinyanga.
Kwa mujibu wa ACP Mgani, siku ya tukio, marehemu
alikuwa akielekea kanisani alfajiri wakati alipovamiwa na kukatwa mgongoni
chini ya bega la kulia ambapo baada ya shambulio hilo, mtuhumiwa alikimbia huku
majeruhi akianguka chini.
"Majeruhi aliokolewa na wasamaria
wema na kukimbizwa hospitalini kwa ajili ya matibabu, lakini kutokana na kuvuja
damu nyingi, alifariki dunia akiwa hospitalini," amesema
ACP Mgani.
Ameongeza kuwa mpaka sasa jeshi la polisi
linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na kuna watu wanaotiliwa shaka, ingawa
bado hawajatajwa rasmi.
ACP Mgani ametoa wito kwa wananchi wa Shinyanga
kuepuka kujichukulia sheria mkononi na badala yake kufuata taratibu za kisheria
katika kutatua migogoro yao.
"Endapo kuna mgogoro wowote,
wananchi wasitumie njia zisizo halali. Kuna vyombo vya sheria kama mahakama na
mabaraza ya ardhi ambavyo vinaweza kusaidia utatuzi wa migogoro hiyo," amesisitiza.
Jeshi la polisi linaendelea na msako wa waliohusika
na tukio hilo, huku likitoa rai kwa yeyote mwenye taarifa kusaidia uchunguzi.
Post a Comment