" JESHI LA POLISI SHINYANGA LAENDELEA NA UCHUNGUZI WA KIFO CHA MWANAMKE MWENYE UALBINO

JESHI LA POLISI SHINYANGA LAENDELEA NA UCHUNGUZI WA KIFO CHA MWANAMKE MWENYE UALBINO

Na Mapuli Kitina Misalaba

Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga linaendelea na uchunguzi wa kifo cha mwanamke mwenye ualbino Wande Mbiti Kulwa (28), mkazi wa kijiji cha Nhelegani, kata ya Kizumbi, Manispaa ya Shinyanga, ambaye mwili wake ulikutwa ndani ya nyumba yake huku mlango ukiwa umefungwa kwa kufuli nje.

Tukio hilo limebainika baada ya wakazi wa eneo hilo kuhisi harufu isiyo ya kawaida, hali iliyosababisha kutoa taarifa kwa viongozi wa mtaa.

Diwani wa kata hiyo, Mhe. Reuben Kitinya, pamoja na uongozi wa kitongoji hicho, wamekiri kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa marehemu alikuwa akiishi peke yake.

Katibu wa Chama cha Watu Wenye Ualbino Manispaa ya Shinyanga, Masanja William, ameonyesha masikitiko yake juu ya tukio hilo na kutoa wito kwa vyombo vya usalama kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini wahusika.

Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Nhelegani wamesema wameshtushwa na tukio hilo na wanaomba uchunguzi wa kina ufanyike ili haki itendeke.

Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Kennedy Mgani, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa tayari uchunguzi wa awali umefanyika, na kwamba  upelelezi unaendelea ili kubaini chanzo cha kifo hicho.

Aidha, amewataka wananchi kuwa na subira wakati vyombo vya dola vikiendelea na uchunguzi wa kina, huku akisisitiza kuwa taarifa zaidi zitatolewa kwa jamii pindi uchunguzi utakapokamilika.

"Ni kweli hilo tukio limetokea. Askari walifika kwenye eneo la tukio wakiwa na daktari, ambapo mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi. Baada ya daktari kujiridhisha, ndugu walipewa mwili kwa ajili ya mazishi ambayo tayari yamefanyika. Upelelezi unaendelea kuhusiana na tukio hili, hivyo ni suala la kulipa muda Jeshi la Polisi na vyombo vingine vinavyohusika ili kubaini kilichotokea. Baadaye jamii itafahamishwa.”ACP Mgani

Kwa mujibu wa taarifa za familia, baba wa marehemu, mzee Mbiti Kulwa, amesema Wande ameacha watoto watatu wa kike na kwamba mara ya mwisho kuonekana ilikuwa Alhamisi, Februari 27, 2025.

Mazishi ya Wande Mbiti Kulwa tayari yamefanyika katika kitongoji hicho.

Post a Comment

Previous Post Next Post