Na Mapuli Kitina Misalaba
Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga linaendelea na
uchunguzi wa kifo cha mwanamke mwenye ualbino Wande Mbiti Kulwa (28), mkazi wa
kijiji cha Nhelegani, kata ya Kizumbi, Manispaa ya Shinyanga, ambaye mwili wake
ulikutwa ndani ya nyumba yake huku mlango ukiwa umefungwa kwa kufuli nje.
Tukio hilo limebainika baada ya wakazi wa eneo hilo
kuhisi harufu isiyo ya kawaida, hali iliyosababisha kutoa taarifa kwa viongozi
wa mtaa.
Diwani wa kata hiyo, Mhe. Reuben Kitinya, pamoja na
uongozi wa kitongoji hicho, wamekiri kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa
marehemu alikuwa akiishi peke yake.
Katibu wa Chama cha Watu Wenye Ualbino Manispaa ya
Shinyanga, Masanja William, ameonyesha masikitiko yake juu ya tukio hilo na
kutoa wito kwa vyombo vya usalama kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini
wahusika.
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Nhelegani wamesema
wameshtushwa na tukio hilo na wanaomba uchunguzi wa kina ufanyike ili haki
itendeke.
Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Jeshi la
Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Kennedy Mgani, amethibitisha kutokea kwa tukio
hilo na kueleza kuwa tayari uchunguzi wa awali umefanyika, na kwamba upelelezi unaendelea ili kubaini chanzo cha
kifo hicho.
Aidha, amewataka wananchi kuwa na subira wakati
vyombo vya dola vikiendelea na uchunguzi wa kina, huku akisisitiza kuwa taarifa
zaidi zitatolewa kwa jamii pindi uchunguzi utakapokamilika.
"Ni kweli hilo tukio limetokea.
Askari walifika kwenye eneo la tukio wakiwa na daktari, ambapo mwili wa
marehemu ulifanyiwa uchunguzi. Baada ya daktari kujiridhisha, ndugu walipewa
mwili kwa ajili ya mazishi ambayo tayari yamefanyika. Upelelezi unaendelea kuhusiana
na tukio hili, hivyo ni suala la kulipa muda Jeshi la Polisi na vyombo vingine
vinavyohusika ili kubaini kilichotokea. Baadaye jamii itafahamishwa.”ACP Mgani
Kwa mujibu wa taarifa za familia, baba wa marehemu,
mzee Mbiti Kulwa, amesema Wande ameacha watoto watatu wa kike na kwamba mara ya
mwisho kuonekana ilikuwa Alhamisi, Februari 27, 2025.
Mazishi ya Wande Mbiti Kulwa tayari yamefanyika katika kitongoji hicho.
Post a Comment