Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linawashikilia
watu wawili kwa tuhuma za mauaji ya Ndani Kasuma mwenye umri wa Miaka 72, mkazi
wa kijiji cha Idodoma, kata ya Samuye, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.
Kaimu Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Shinyanga, ACP Kennedy Mgani, amesema tukio hilo limetokea Machi 3,
2025, majira ya saa tatu kuelekea saa nne usiku, wakati marehemu akiwa nje ya
nyumba yake akipata chakula cha usiku na binti yake.
"Walivamiwa
na watu waliokuwa na silaha zenye ncha kali, ambapo marehemu alijeruhiwa
kichwani na kisogoni. Ingawa waliwatambua kwa sura, washambuliaji walikimbia
baada ya kufanya tukio hilo. Jitihada za kumuwahisha hospitalini hazikufua
dafu, kwani alifariki usiku huo huo," amesema ACP
Mgani.
Ameeleza kuwa uchunguzi
wa awali umebaini kuwa mgogoro wa ardhi huenda ndiyo chanzo cha tukio hilo,
kwani marehemu alikuwa na mgogoro na watu hao hadi kufikia hatua ya kufungua
mashauri katika baraza la ardhi la wilaya.
"Watu
wawili tayari tumewashikilia na tunaendelea kuwasaka wengine waliohusika.
Tutahakikisha wote wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria,"
amesema.
Jeshi la Polisi limewataka wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kufuata taratibu za kisheria katika kutatua migogoro yao badala ya kujichukulia sheria mkononi.
Post a Comment