
Na Halima Issa, Misalaba Media
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini
imekagua ujenzi wa jengo la Wizara ya Nishati katika mji wa Serikali Mtumba na
kuipongeza Wizara kwa hatua ya ujenzi iliyofikiwa kwa asilimia 94.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. David Mathayo
amesema hayo tarehe 20 Machi 2025, wakati wa ziara ya kukagua ujenzi wa jengo
hilo katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma iliyohusisha Menejimenti ya
Wizara na baadhi ya watumishi.
“Tumepita
kila mahali katika jengo hilo kazi nzuri na kubwa imefanyika na mandhari ya
ndani na ya nje zote zinavutia sana, nawapongeza sana Wizara ya Nishati kwa
kazi hii, zaidi kamati inampongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa
kuhakikisha kuwa fedha zinapatikana za kutekeleza ujenzi wa majengo mengi na
mazuri ya serikali.”Amesema Mathayo
Amepongeza Viongozi Wakuu na Menejimenti ya Wizara
ya Nishati kwa kusimamia vyema ujenzi huo na kuhakikisha fedha za mkandarasi zinalipwa
kwa wakati wakati wote.
Aidha,amewasisitiza kukamilisha kazi ndogo
zilizosalia ili watumishi waweze kuhamia katika jengo hilo mapema.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya
Nishati, Dkt. Khatibu Kazungu, amesema kuwa watumishi wa Wizara ya Nishati
wanatarajia kuhamia katika jengo hilo kabla ya mwezi Mei 2025 kwa kuwa kazi
kubwa tayari imeshafanyika.


Post a Comment