" KATIBU WA CCM MKOA WA SHINYANGA ODILIA BATIMAYO AFUTURISHA VIONGOZI WA DINI, WAUMINI NA WANANCHI WA SHINYANGA

KATIBU WA CCM MKOA WA SHINYANGA ODILIA BATIMAYO AFUTURISHA VIONGOZI WA DINI, WAUMINI NA WANANCHI WA SHINYANGA


Na Mapuli Kitina Misalaba

Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga, Odilia Batimayo, Machi 28, 2025, amefuturisha viongozi wa dini, waumini, na wananchi wa Shinyanga, huku akisisitiza mshikamano na maombi kwa taifa katika kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Hafla hiyo imefanyika mjini Shinyanga, ikiambatana na dua maalum iliyoongozwa na Sheikh wa Mkoa wa Shinyanga, Ismail Makusanya, ambapo maombi yameelekezwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2025, amani ya taifa, pamoja na ustawi wa jamii kwa ujumla.

Katika dua hiyo, Sheikh Makusanya pia amemwombea Katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Odilia Batimayo, akimuomba Mwenyezi Mungu aendelee kumbariki, kumlinda, na kumpa nafasi ya juu zaidi katika majukumu yake ya uongozi.

“Katika kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, tunapaswa kutafakari umuhimu wa maombi kwa viongozi wetu na taifa kwa ujumla, tukiamini kwamba baraka za Mwenyezi Mungu zinaweza kuleta mwelekeo mzuri katika hatima ya nchi yetu”.amesema Sheikh Makusanya

Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Odilia Batimayo, amewashukuru viongozi wa dini kwa ushirikiano wao na kuwaomba waendelee kudumisha mshikamano, hasa katika kipindi hiki kinachoelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Pia ameahidi kuwa chama hicho kitaendelea kushirikiana nao kwa karibu ili kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kutawala.

Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini, wakiwemo:

Sheikh wa Wilaya ya Shinyanga Soud Kategile, Maimamu na Masheikh wa Kata (BAKWATA), Wajumbe wa Baraza la Halmashauri Kuu (BAKWATA) Mkoa wa Shinyanga, Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu (JUWAKITA) Mkoa wa Shinyanga, Taasisi ya Istiqama, MDB, Isuwat, Zawiya, JUVIKIBA Wilaya ya Shinyanga, Wazee wa dini na viongozi wa taasisi za Kiislamu

Hafla hiyo imeendelea kuwa ishara ya mshikamano kati ya viongozi wa kisiasa na wa dini, hususan katika kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhani, ambapo amani na maombi yanazidi kupewa kipaumbele kwa ustawi wa taifa.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post