Katibu wa Jumuiya ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Kanda ya Ziwa, Shujaa Daniel Kapaya, amewataka Mashujaa wa SMAUJATA kuwa wazalendo katika kutekeleza majukumu yao, huku akisisitiza ubunifu kwa kila kiongozi wa idara ili kuhakikisha malengo ya jumuiya yanatimia.
Akizungumza katika kikao kazi kilichofanyika katika Chuo cha Ufundi kwa Watu Wenye Ulemavu Mirongo, Mwanza, Shujaa Kapaya amesema SMAUJATA imepanua wigo wake kwa kuanzisha idara mbalimbali, hivyo kila kiongozi anapaswa kuhakikisha anasimamia vyema majukumu yake kwa ubunifu na ufanisi.
Aidha, amegusia suala la utoaji wa vitambulisho kwa Mashujaa na kusisitiza umuhimu wa kutoa elimu kwa jamii kuhusu kupinga ukatili.
Pia, amehimiza mashirikiano kati ya SMAUJATA na idara zote za serikali ili kuimarisha mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili katika jamii.
Kikao hicho kimehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mwenyekiti wa SMAUJATA Mkoa wa Mwanza, Shujaa Gasto Alex Didasi, viongozi wa kitaifa Kamishna wa SMAUJATA Taifa, Shujaa Nyaido Mussa Mganga, ambaye aliwapongeza Mashujaa wa Mwanza kwa juhudi zao katika kupambana na vitendo vya ukatili.
Katika kikao hicho, Shujaa Godfrey Julius amekabidhiwa rasmi ofisi ya Unaibu Katibu, huku Kamishna Nyaido Mussa akimkabidhi majukumu ya Makamu Mwenyekiti wa SMAUJATA Mkoa wa Mwanza, Shujaa Agripiner Faustine Mussita.
Uteuzi wa viongozi hao ulifanywa na Mwenyekiti wa SMAUJATA Taifa, Shujaa Sospeter Mosewe Bulugu.
"KATAA UKATILI, WEWE NI SHUJAA!"
Post a Comment