
Na Mapuli Kitina Misalaba
Waandishi wa habari nchini wametakiwa kuzingatia
misingi ya taaluma yao, weledi na maadili katika kutekeleza majukumu yao, hasa
katika kuelekea uchaguzi mkuu.
Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, ambaye pia ni
Mkurugenzi Msaidizi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Renatus Mkude, amesema hayo
leo Machi 14, 2025, katika Mkutano wa Wadau wa Taasisi ya Vyombo vya Habari
Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA-TAN), uliofanyika jijini Dodoma.
Mkude amesisitiza umuhimu wa waandishi wa habari
kutumia kalamu zao kwa uadilifu na kuzingatia misingi ya taaluma kwa manufaa ya
jamii na ustawi wa taifa. "Ni wajibu wa kila mwandishi kuhakikisha kuwa
habari zinazoripotiwa zinazingatia ukweli, usahihi na maadili ya taaluma ya
habari," amesema.
Moja ya maazimio ya kongamano hilo ni kuhakikisha
kuwa vyombo vya habari vinaanza kuzingatia habari za maendeleo na kuimarisha
ushirikiano na wadau mbalimbali.
Kongamano hilo limependekeza kuanzishwa kwa vituo
maalum vya mafunzo kwa waandishi wa habari kuelekea uchaguzi mkuu, ili
kuwaandaa kwa weledi katika kuripoti habari za uchaguzi.
Pia tasnia ya habari inapaswa kuanza mchakato wa
kuripoti habari za uchaguzi mapema – kabla, wakati na baada ya uchaguzi huku Sauti
za wananchi zinapaswa kupewa kipaumbele katika habari za uchaguzi.
Aidha, MISA-TAN imetakiwa kuandaa semina maalum kwa
waandishi wa habari kuhusu masuala ya uchaguzi, huku kila klabu za waandishi wa
habari nchini zikihimizwa kuunda timu maalum za kuripoti habari za uchaguzi.
Katika kuhakikisha waandishi wanatekeleza majukumu
yao kwa uhuru, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imependekezwa kufanya
mazungumzo na Jeshi la Polisi ili kuweka utaratibu wa kulinda haki za wanahabari
wakati wa uchaguzi.
Katika mkutano huo, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa
Watumishi wa Umma (PSSSF) umeeleza namna unavyoendelea kuimarisha mchango wake
katika kukuza uchumi wa taifa kwa kuboresha uwekezaji wake.
Mwanasheria Mkuu wa PSSSF, Valentino Maganga,
amesema mfuko huo umeongeza kiwango cha maendeleo kutoka asilimia 22 mwaka 2023
hadi asilimia 36 mwaka 2024/2025, huku ukilenga kufikia asilimia 40 kwa ajili
ya kuimarisha uchumi wa Tanzania.
Maganga amesema PSSSF imeongeza thamani ya uwekezaji
wake kutoka trilioni 6 hadi trilioni 10, huku dhamana za uwekezaji zilizopo
kwenye taasisi za kifedha kama benki na majumba, zenye thamani ya Shilingi
Trilioni 9, zikichangia katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
"PSSSF
inalipa pensheni kwa wastafu kila mwezi kiasi cha Shilingi Bilioni 70, na kwa
mwaka ni zaidi ya Shilingi Bilioni 800. Fedha hizi huchochea shughuli za uchumi
na kusaidia katika uwekezaji unaoingizia mapato serikali,"
amesema Maganga.
Meneja wa Kitengo cha Utangazaji wa Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mhandisi Andrew Kisaka, amewataka waandishi wa
habari na vyombo vya habari kuzingatia maadili ya uandishi na utangazaji, hasa
wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu.
Akizungumza katika kongamano hilo, Mhandisi Kisaka
amesema vyombo vya habari vinapaswa kufanya kazi kwa haki, usawa na uadilifu,
na kuhakikisha kuwa vyama vyote vya siasa vinapewa nafasi sawa katika
kuripotiwa.
"Ni
muhimu kwa waandishi wa habari kutenda haki kwa kuripoti kile kilichotokea kama
kilivyokuwa, bila kuongeza chumvi au kufanya utani kwenye habari. Vyombo vya
habari vina wajibu wa kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na
zinazowawezesha kufanya maamuzi ya busara,"
amesema Kisaka.
Pia amesisitiza kuwa waandishi wanapaswa kuepuka
kuripoti habari zisizo za kweli na badala yake wajikite zaidi katika kuripoti
sera na ahadi za vyama vya siasa, ili kuwasaidia wananchi kuelewa mipango ya
vyama na jinsi wanavyokusudia kutatua changamoto zilizopo.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini
mwa Afrika – Tanzania (MISA-TAN), Edwin Soko, amewashukuru wadau wa habari na
taasisi mbalimbali kwa kufanikisha mkutano huo.
Miongoni mwa taasisi zilizojitokeza kufadhili
mkutano huo ni Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Hifadhi ya
Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF), Mfuko wa
Maendeleo ya Jamii (TASAF), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), na Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB).
Taasisi nyingine ni Shirika la TASHICO, Tanzania
Human Rights Defenders Coalition (THRDC), na Pan-African Constructive
Journalism Initiative (PACJI), ambazo ushiriki wao unatarajiwa kuleta mchango
mkubwa katika kuboresha tasnia ya habari nchini.
Wakati huo huo Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini
mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA-TAN), imewatunuku tuzo za heshima wajumbe wa
bodi waliomaliza muda wao kama ishara ya kutambua mchango wao katika uongozi wa
taasisi hiyo.
Bodi hiyo iliyomaliza muda wake ilihudumu kwa miaka
minane hadi uchaguzi wa viongozi wapya uliofanyika Desemba 4, 2024, ambapo
Edwin Soko alichaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa MISA-TAN.
Miongoni mwa waliotunukiwa ni Salome Kitomari
(Mwenyekiti wa zamani), James Malenga (Makamu Mwenyekiti), pamoja na wajumbe
Mussa Juma, Michael Gwimila, na Idda Mushi.
Aidha, katika mkutano huo, MISA-TAN pia imetoa vyeti
vya pongezi kwa wadau wake wakuu, wakiwemo PSSSF, NSSF, TCRA, PCCB, TASAF,
TASHICO, NHIF, THRDC, na PAN-AFRICAN, kwa mchango wao katika kuimarisha sekta
ya habari nchini.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA! 🍷🍸
Post a Comment