MAWAKALA WA VYAMA KIELELEZO CHA UWAZI UBORESHAJI DAFTARI LA WAPIGA KURA
Map0
Na. Mwandishi Wetu Uwepo wa mawakala wa vyama vya siasa wakati
wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ni kielelezo cha uwazi na ni
muhimu kwa kuwa mawakala hao watasaidia kutambua waombaji wa eneo husika hivyo
kupunguza kutokea kwa vurugu zisizokuwa za lazima. Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya
Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele leo tarehe 06 Machi,
2025 wakati akifungua mafunzo ya watendaji wa uboreshaji wa Daftari wa mkoa wa
Dar es Salaam. Jaji Mwambegele amesema licha ya umuhimu huo
mawakala hao wa vyama vya siasa hawaruhusiwi kuwaingilia watendaji wakati wote
wa utekelezaji wa majukumu yao vituoni. “Wakati wa uboreshaji wa Daftari mawakala wa
vyama vya siasa wataruhusiwa kuwepo katika vituo vya kuandikisha wapiga
kura.Jambo hili ni muhimu kwani
litasaidia kuleta uwazi katika zoezi zima lakini pia mawakala hao watasaidia
kutambua waombaji wa eneo husika hivyo kupunguza kutokea kwa vurugu zisizokuwa
za lazima,” amesema. Katika hatua nyingine, Jaji Mwambegele
amesema Tume imetoa kibali kwa asasi za kiraia 157 kwa ajili ya kutoa elimu ya
mpiga kura na kibali kwa taasisi na asasi za kiraia 42 kuwa waangalizi
watakaoshiriki katika zoezi la uboreshaji wa Daftari ambapo kati ya hizo,
taasisi tisa ni za kimataifa na 33 ni za ndani ya nchi. Amewasisitiza watendaji hao kutoa ushirikiano
kwa taasisi, asasi na waangalizi waliopata vibali watakapofika kwenye maeneo
yao kwa kuwa ni wadau muhimu na akaongeza kuwa Tume itawapa vitambulisho kwa
urahisi wa kuwatambua. Jaji Mwambegele amewataka watendaji hao
kutekeleza majukumu yao kwa umakini katika kila eneo ikiwemo utunzaji wa vifaa
vya uandikishaji kwa kuwa vifaa hivyo vimenunuliwa kwa gharama kubwa na
vinatakiwa kutumika katika awamu ya pili ya uboreshaji wa Daftari. “Kutokuwa makini katika utunzaji wa vifaa
hivi kutapelekea athari kubwa katika ukamilishaji wa zoezi hili muhimu. Aidha,
mnapaswa kuzingatia maelekezo yote yatakayotolewa na Tume ili muweze kuyafanyia
kazi wakati zoezi litakapokuwa limeanza,” amesema. Mafunzo hayo ni sehemu ya maandalizi ya
uboreshaji wa Daftari mkoani Dar es Salaam ambao utaanza tarehe 17 hadi 23
Machi, 2025 ambapo vituo vitakuwa vinafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na
kufungwa saa 12:00 jioni.
Mwenyekiti
wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele
akijadili jambo na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume, Ndg. Kailima Ramadhani
(kulia) wakati wa mafunzo ya siku mbili kwa mafunzo ya watendaji wa uboreshaji
wa Daftari wa mkoa wa Dar es Salaam yaliyoanza leo Machi 06,2025 na yanataraji
kumalizika kesho Machi 07, 2025 na kufanyika Ubungo mkoani Dar es salaam.
Mkaguzi Msaidizi wa Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salaam, Christophrer Anania akiwasilisha mada ya uraia.
Washiriki wakiwa katika ufunguzi wa mafunzo hayo.
Washiriki wakila kiapo cha kujitoa uanachama na kutunza siri kabla ya kuanza mafunzo hayo ya siku mbili ikiwa ni maandaliazi ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mkoa wa Dar es Salaam.
Safari ya Ladha: Ubora wa East African Spirits (T) Ltd
Post a Comment