" MKUTANO MKUU WA CHAMA CHA WALIMU (CWT) WILAYA YA SHINYANGA WAFANYIKA, DC MTATIRO AWATAKA WALIMU KUZINGATIA MAADILI YA KAZI

MKUTANO MKUU WA CHAMA CHA WALIMU (CWT) WILAYA YA SHINYANGA WAFANYIKA, DC MTATIRO AWATAKA WALIMU KUZINGATIA MAADILI YA KAZI

Mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, akifungua mkutano mkuu wa Chama cha Walimu (CWT) Wilaya ya Shinyanga leo Machi 21, 2025.


Na Mapuli Kitina Misalaba

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, amewataka walimu kuzingatia misingi na taratibu zilizopo katika utekelezaji wa majukumu yao.

 Akizungumza katika mkutano mkuu wa Chama cha Walimu (CWT) Wilaya ya Shinyanga, pamoja na mambo mengine DC Mtatiro amewahimiza walimu kujiepusha na mikopo yenye riba kubwa ambayo mara nyingi husababisha migogoro sehemu za kazi.

Amesisitiza kuwa walimu wanapaswa kuwa makini katika masuala ya kifedha ili kuepuka matatizo yanayoweza kuathiri utendaji wao wa kazi.

Aidha, ameendelea kuwasisitiza walimu kujenga tabia ya kufanya mazoezi mara kwa mara ili kuimarisha afya zao na kuepukana na magonjwa yanayotokana na ukosefu wa mazoezi, kama vile shinikizo la damu na kisukari.

Katibu wa CWT Wilaya ya Shinyanga, Rose Mboneko, akisoma risala kwa mgeni rasmi, ameeleza kuwa chama hicho kitaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi.

Amesema miongoni mwa majukumu hayo ni kufundisha wanafunzi, kutetea maslahi ya walimu, kushiriki kazi mbalimbali za kitaifa, kutoa huduma za kisheria kwa wanachama, kuwahamasisha walimu kujiendeleza kitaaluma, na kuhimiza ufaulu wa wanafunzi.

Hata hivyo, Mboneko ametaja changamoto zinazowakabili walimu, zikiwemo Madeni ya mshahara na yasiyo ya mshahara kutolipwa kwa wakati, Upungufu wa nyumba za walimu, Ukosefu wa mafunzo ya kutosha kuhusu mitaala mipya, Upungufu wa walimu katika baadhi ya shule pamoja na Vikokotoo visivyo rafiki kwa walimu wastaafu.

Katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Wanawake CWT Wilaya ya Shinyanga Rose Mabana amesoma taarifa ya utendaji wa chama kwa kipindi cha miaka miwili na nusu, kuanzia Oktoba 2022 hadi Machi 2025.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa chama kimefanikiwa kutekeleza malengo yake, ikiwa ni pamoja na Uboreshaji wa huduma kwa wanachama, Usajili wa wanachama wapya, Ufuatiliaji wa madeni ya mishahara na yasiyo ya mishahara ambapo serikali imeendelea kulipa madeni hayo, Kutoa elimu ya wafanyakazi kwa walimu mahala pa kazi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wilaya ya Shinyanga ina walimu wa shule za msingi na sekondari jumla ya 1,064, ambapo wanachama wa CWT ni 945. Walimu wasiokuwa wanachama ni 119, huku idadi ya walimu wanaume ikiwa 458 na wanawake 606.

Mkutano huo pia umehusisha uchaguzi wa viongozi mbalimbali wa chama, wakiwemo Mwenyekiti wa CWT Wilaya ya Shinyanga pamoja na wawakilishi wa shule za msingi na sekondari. Uchaguzi huo ni sehemu ya utaratibu wa chama wa kuhakikisha uongozi wake unasimamiwa kwa uwazi na uwajibikaji.

Mwenyekiti wa CWT Mkoa wa Shinyanga Mwalimu Mathias Balele imewakumbusha walimu kuhusu wajibu wao wa kufuata maadili ya kazi, sheria za nchi, katiba na kanuni za chama.

Mwalimu Balele amesema ni muhimu walimu kuendelea  kushirikiana kwa pamoja ili kuimarisha mshikamano wao kwa manufaa ya chama na wanachama wake.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi CCM Wilaya ya Shinyanga mjini Mhe. Anord Makombe amewaasa walimu hao kujiepusha na makundi baada ya uchaguzi huo ambapo amewahimiza kuendelea kuwa wamoja ili kufikia malengo yao.

Mkutano huu wa CWT Wilaya ya Shinyanga hufanyika kila baada ya miaka miwili na unatoa fursa kwa walimu kujadili changamoto zao na kutafuta suluhisho kwa pamoja.

Kauli mbiu ya CWT ni: WAJIBU NA HAKI.

Mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, akizungumza katika mkutano wa Chama cha Walimu (CWT) Wilaya ya Shinyanga leo Machi 21, 2025.

Mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, akizungumza katika mkutano wa Chama cha Walimu (CWT) Wilaya ya Shinyanga leo Machi 21, 2025.

Mkutano mkuu wa Chama cha Walimu (CWT) Wilaya ya Shinyanga ukiendelea leo Machi 21, 2025 katika ukumbi wa mikutano SHYCOM.





TAZAMA VIDEO 

 

Post a Comment

Previous Post Next Post