Na Mapuli Kitina Misalaba
Kifuatia tukio la Mwanamke mwenye ualbino, Wande
Mbiti Kulwa (38), mkazi wa kijiji cha Nhelegani, kata ya Kizumbi, Manispaa ya
Shinyanga, kukutwa amefariki dunia ndani ya nyumba yake huku mlango ukiwa
umefungwa kwa kufuli nje, ambapo hali hiyo inazua maswali kuhusu mazingira ya
kifo chake.
Tukio hilo limeibua taharuki miongoni mwa wakazi wa
eneo hilo, huku vikosi vya usalama vikiendelea na uchunguzi wa kina kubaini
kilichotokea.
Akizungumza na Misalaba Media, aliyewahi kuwa mwenyekiti wa chama cha
waganga wa tiba asili Mkoa wa Shinyanga Mzee Idd Mpyalimi, ameeleza kuwa imani
za baadhi ya watu kuhusisha viungo vya watu wenye ualbino na utajiri ni potofu
na zinachochewa na umaskini pamoja na udanganyifu wa waganga matapeli.
“Nimefanya
utafiti kwa muda mrefu na kubaini kuwa hakuna biashara yoyote inayohusiana na
viungo vya watu wenye ualbino. Ni imani potofu zinazochangiwa na hali ngumu ya
maisha, ambapo watu wengi huaminishwa uongo na kuishia kupoteza pesa zao.
Waganga wa tiba asili halali hawawezi kuhusika na upuuzi kama huo,”
amesema Mzee Mpyalimi.
Aidha, amewataka wananchi kutoamini maneno ya
matapeli wanaodai kuwa viungo vya watu wenye ualbino vinaweza kuleta utajiri.
“Mganga wa tiba asili akikwambia ufanye hivyo, huyo ni tapeli, ni bora
ukamlipoti polisi,” ameongeza.
Hadi sasa, jeshi la polisi mkoani Shinyanga
linaendelea na uchunguzi wa kifo cha Wande Mbiti Kulwa ili kubaini chanzo cha
tukio hilo.
Post a Comment