Na. Paul Kasembo, SHY RS.
MHE. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa zawadi
mbalimbali kwa Makao ya Watoto Yatima (Shinyanga Society For Orphans) iliyopo
Bushushu na Makazi ya Wazee na Wenye
Mahitaji Maalum Kolandoto iliyopo Kata ya Kolandoto zote zikiwa Halmashauri ya
Manispaa ya Shinyanga.
Akizungumza baada ya kukabidhi Mkuu wa Mkoa wa
Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amesema kuwa ikiwa ni kuelekea katika Sikukuu ya
Eid Al - Fitr, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatambua, anathamini na
kuheshimu uwepo wa wao na kwamba yeye mwenyewe na Serikali yake anawapenda na
kuwajali wakati wote ndiyo sababu ya kuwapelekea zawadi hizo kwani wao pia ni
jamii kama ilivyo jamii nyingine na wanazo haki sawasawa kama binadamu wengine.
"Tunapoelekea katika kuhitimisha Mfungo Mtukufu
wa Mwezi wa Ramadhan, nimeelekezwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania niwaletee zawadi zake alizotoa maalum kwa ajili
yenu ili katika kusherehekea Sikukuu hii ya Eid Al - Fitr muweze kufurahi
pamoja naye kupitia zawadi hizi," alisema RC Macha.
"Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan
anatambua, anathamini na kuheshimu uwepo wenu na kwamba Serikali anayoiongoza
itaendelea kuwa karibu na kuishi nanyi wakati wote, aidha itaendelea
kusaidizana nanyi katika nyanja na nyakati mbalimbali kutegemea na mahitaji ya
wakati husika pia," alisisitiza RC Macha
Kwa nyakati tofauti Mkurugenzi wa Makao ya Watoto
Bibi Haiyamu Said na Msimamizi wa Makazi ya Wazee na Wenye Mahitaji Maalum Bi. Sophia Kang'ombe
wamemshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwathamini,
kuwajali na hata kuwapatia zawadi mbalimbali nyakati zote kupitia wasaidizi
wake (Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga) na kwamba wao wanamuombea kwa Mwenyezi Mungu
awe na afya njema wakati wote ili andelee kuwahudumia wao na Watanzania wote.


Post a Comment