" RC MACHA AJUMUIKA NA WANASHINYANGA KUMUOMBEA DUA RAIS DKT. SAMIA SULUHU HASSAN

RC MACHA AJUMUIKA NA WANASHINYANGA KUMUOMBEA DUA RAIS DKT. SAMIA SULUHU HASSAN

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Anamringi Macha, akizungumza leo Machi 29, 2025.

Na Mapuli Kitina Misalaba

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Anamringi Macha, leo Machi 29, 2025 amefuturisha viongozi wa serikali, dini, siasa, makundi mbalimbali ya watoto wenye uhitaji, na wananchi kwa ujumla.

Katika hafla hiyo, Sheikh wa Mkoa wa Shinyanga, Ismail Makusanya, ameongoza dua maalum kwa ajili ya kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ili Mungu aendelee kumlinda, kumtangulia na kumuepusha na mabaya katika utekelezaji wa majukumu yake ya uongozi.

Dua hiyo pia imehusisha maombi ya kuendelea kudumisha amani, utulivu, na usalama nchini, pamoja na kuombea  uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 ufanyike kwa amani, na viongozi waadilifu wapate nafasi ya kuhudumu katika majimbo na kata mbalimbali kwa mujibu wa katiba.

Aidha, Sheikh Makusanya ametumia nafasi hiyo kumuombea Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Anamringi Macha, pamoja na ustawi wa mkoa huo kwa ujumla huku akimpongeza kwa jitihada zake katika kuwatumikia wananchi na kuhakikisha maendeleo yanaendelea kuimarika.

Akizungumza katika hafla hiyo, RC Macha amewashukuru wafanyabiashara wa Shinyanga kwa kuitikia wito wake wa kuhakikisha bei za vyakula hazipandi wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

"Mwaka huu tumeshuhudia tofauti kubwa ukilinganisha na miaka mingine, kwani bei za vyakula hazijabadilika kabisa. Mimi pamoja na wakuu wa wilaya tumefuatilia kwa umakini na tumeridhika na hali hii," amesema RC Macha

Pia amewapongeza wanasiasa wa mkoa wa Shinyanga kwa kuzingatia makubaliano ya kutofanya futari za kisiasa kipindi chote cha Ramadhani, akiwataka waendelee kuzingatia utulivu na mshikamano kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025.

Kuhusu sikukuu ya Eid, RC Macha amewatakia Waislamu na wananchi wote sherehe njema, huku akisisitiza umuhimu wa kudumisha usalama.

"Serikali imejiandaa kuhakikisha kwamba amani na usalama vinakuwepo, lakini ni jukumu la wazazi pia kuwa makini na watoto wao wasizurure hovyo katika maeneo ya sherehe," amesema Macha

Aidha, amewaonya wafanyabiashara wanaotumia sikukuu kuuza vinywaji vilivyoisha muda wa matumizi, akisema hatua kali zitachukuliwa kwa watakaobainika.

Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mhe. Mboni Mhita, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Peter Masindi, viongozi wa vyama vya siasa, wakurugenzi wa Halmashauri, na watumishi wa serikali kutoka Manispaa ya Shinyanga.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Anamringi Macha, akizungumza leo Machi 29, 2025.

Sheikh wa Mkoa wa Shinyanga, Ismail Makusanya, akiongoza dua maalum kwa ajili ya kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Machi 29, 2025 wakati wa hafla ya futari ambayo imeandaliwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha.

Post a Comment

Previous Post Next Post