" SERIKALI IMELETA ZAIDI YA BILLION 18 KWA AJILI YA KUTEKELEZA MIRADI YA MAJI.

SERIKALI IMELETA ZAIDI YA BILLION 18 KWA AJILI YA KUTEKELEZA MIRADI YA MAJI.


MKUU wa Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza , Johari Samizi amesema serikali imeleta zaidi ya bilion 18 katika eneo hilo kwa ajili kutekeleza miradi 20 ya maji hivyo kumtua mama ndoo kichwani na kukamilika kwake kutavuka lengo la upatikanaji maji kwa asilimia 85.

Samizi amesema hayo jana katika eneo hilo kuwa fedha hizo zimefika wilayani hapo na wakandarasi wako kazini wakitekeleza ujenzi wa miradi hiyo ambayo imepangwa yote kukamilika hapo mwezi Oktoba mwaka huu.

Alitoa wito kwa wananchi katika wilaya hiyo kutunza miradi hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu huku akisistiza kwa makundi ya usimamizi wa maji katika vijiji kuwa na utaratibu mzuri wa kukusanya fedha zinazopatikana kwa huduma hiyo ili ziwezeshe uendelevu wa huduma hiyo.

Samizi aliongeza kusema kuwa wilaya hiyo kwa sasa upatikanaji wa maji uko asilimia 73 ambapo lengo la serikali hadi mwaka huu liwe ni asilimia 85 hivyo kutokana na kuwepo kwa juhudi pamoja na kupatikana kwa fedha za miradi hiyo kukamilika kwake kutawezesha eneo hilo kufikisha asilimia 89.2 na kuvuka lengo.

"Napongeza juhudi zilizofanywa na serikali ya awamu ya sita amabazo hadi sasa zimewezesha wilaya yetu kupokea zaidi ya bilion 73 katika kipindi cha uongozi wa rais wetu kwa ajili ya miradi ya maji" alisema Samizi.

Wakati huo huo Mkuu wa Wilaya hiyo alisema wajasiriamali katika eneo hilo wamekopeshwa zaidi ya milioni  398.7 kwa ajili ya kuendeshea shughuli zao ambapo baada ya kusimama kwa zoezi la utoaji wa mikopo wakopaji hao waliweza kurejesha milioni 127.

Samizi amevitaka vikundi 41 vilivyopata mikopo hiyo kuzitumia katika miradi waliyoombea ili waweze kupata faida na hivyo kujiletea maendeleo yao kwa haraka na kuondoa ugumu wa maisha.

Alisema wilaya hiyo kutokana na makusanyo yake ya ndani vilevile imeweza kutenga asilimia 40 na kuzitumia kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, zahanati na matundu ya choo.

Samizi alisema hatua hiyo imewezesha wanafunzi kuweza kusoma karibu na maeneo yao huku kwa huduma za matibabu wananchi kwa sasa hawatembei umbali mrefu.

Post a Comment

Previous Post Next Post