
Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga Nyakia Ally Chirukile wakati akikagua mazingira katika moja ya nyumba za kulala wageni

Na Neema Mtuka Sumbawanga,
Rukwa :Serikali imewataka wamiliki wa nyumba za kulala wageni pamoja na maeneo ya starehe kuhakikisha wanazingatia usafi wa mazingira kwa kuepuka kutiririsha maji taka ovyo, sanjari na kuimarisha miundombinu ya vyoo na mfumo wa maji taka ili kulinda afya za Wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Nyakia Ally Chirukile amekemea vikali kwa wale wanaoshiriki uchafuzi wa mazingira kwa makusudi, hususan utiririshaji wa maji taka na utupaji wa taka ovyo katika vichochoro na maeneo ya wazi.
Nyakia ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake na kamati ya usalama wilaya ya Sumbawanga katika ukaguzi wa hali ya mazingira katika Kata ya Katandala ikiwa ni jitihada za kuhakikisha mji unakuwa safi na salama wakati wote.
Mwenyekiti wa mtaa wa jangwani Ramadhan Fan Kabea ameeleza kuwa baadhi ya wamiliki wa nyumba wamekuwa wakiacha maeneo ya nje ya nyumba zao yakiwa machafu bila kuyafanyia usafi na kuhakikisha usafi wa kudumu, hali inayochangia kuongezeka kwa uchafu wa mazingira.
Baadhi ya wananchi akiwemo Lusia Mwambungu amesema kuwa uchafuzi wa mazingira katika vichochoro na mitaro ni hatari kwa afya na unatishia maisha pamoja na ustawi wa jamii huku akiiomba serikali kuendelea kuchukua hatua madhubuti dhidi ya wale wote wanaokaidi maagizo ya kudumisha usafi wa mazingira.
“Suala la usafi wa mazingira ni jukumu la kila mtu kusafisha mazingira yanayomzunguka na kuacha tabia ya kutiririsha maji machafu mamlaka husika zitoe adhabu kali ili kukomesha tabia hiyo”amesema Mwambungu.
Kwa upande wake mmiliki wa nyumba ya kulala wageni Juma Ngajiro amesema kuwa suala la usafi ni muhimu kwa afya za wateja wao hivyo watahakikisha wanazingatia usafi kwa maeneo yote yanayozunguka nyumba hiyo kwa kufanya usafi mara kwa mara ili kujiepusha na magonjwa yatokanayo na uchafu.
Meshach Sichalwe ni muhudumu katika moja ya nyumba za kulala wageni amesema kuwa watahakikisha wanazingatia usafi katika kipindi hiki cha msimu wa mvua ambapo magonjwa mengi ya mlipuko hutokea na hurudisha nyuma maendeleo yao.
Kevin Wilombe ambaye ni mteja katika moja ya nyumba za kulala wageni amesema kuwa jumamosi ya mwisho wa mwezi iliyotengwa kwa ajili ya kufanya usafi pekee haitoshi bali usafi wa mazingira unapaswa kufanywa mara kwa mara.
Amesema kipindi hiki cha mvua kuna baadhi ya watu wanatiririsha maji machafu jambo ambalo ni hatari kwa afya zao na kuzitaka mamlaka husika kuwa na sheria kali na kulipisha gharama kubwa ili kutokomeza tabia hiyo.
“Ni muhimu kuangalia afya zetu kwa kutunza mazingira yanayotuzunguka kwani watoto wadogo huchezea maji machafu jambo linaloweza kusababisha magonjwa ya mlipuko kwa jamii”.amesisitizaWilombe
Serikali inaendelea kusisitiza kuwa usafi wa mazingira ni jukumu la kila mwananchi na hivyo ni muhimu kwa wamiliki wa nyumba za wageni na maeneo ya starehe kushirikiana na mamlaka za usafi ili kuhakikisha mazingira yanakuwa safi, salama, na rafiki kwa maendeleo ya Mji wa Sumbawanga.



Post a Comment