Na Mapuli Kitina Misalaba
Daktari Godfrey Maige kutoka Idara ya Magonjwa ya
Ndani katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga amewatoa hofu wananchi
kuhusu ugonjwa wa homa ya nyani (Mpox), akisisitiza kuwa hakuna mgonjwa
aliyethibitishwa kuwa na ugonjwa huo katika hospitali hiyo hadi sasa.
Ameyasema hay oleo Machi 19, 2025 wakati
akiwasilisha mada ya ugonjwa huo kwa watumishi katika Hospitali hiyo ambapo pamoja
na mambo mengine amesema ugonjwa wa homa ya nyani husababishwa na virusi
vinavyoitwa virusi vya nyani, ambavyo kwa mara ya kwanza viligunduliwa kwa
nyani.
Amesema kuwa mgonjwa mwenye ugonjwa huu huanza kupata
dalili kati ya siku ya kwanza hadi ya tano, dalili zinazofanana na mafua kama
vile homa, maumivu ya misuli, na uvimbe wa tezi hasa kwenye shingo.
“Dalili
nyingine ni vipele vinavyoanzia usoni na kusambaa mwilini, ambavyo baadaye
hugeuka vidonda,” amesema Dkt. Maige.
Hata hivyo, Dkt. Maige ameeleza kuwa ugonjwa huo
unaweza kushindwa na kinga ya mwili bila hata ya matibabu maalum ambapo
ameeleza kuwa hadi sasa hakuna mgonjwa yeyote aliyethibitishwa kuwa na homa ya
nyani katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, hivyo wananchi wasiwe na
hofu.
“Niwatoe
hofu wananchi wa Mkoa wa Shinyanga na maeneo jirani kwamba siyo kila mtu mwenye
vipele ana homa ya nyani. Pia niwasihi wananchi kupata taarifa kutoka vyanzo
vya kuaminika na kushirikiana na mamlaka kama ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa kwa
maelezo sahihi,” amesema Dkt. Maige.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya
Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Luzila John, amewataka watumishi wa afya kuwa
tayari na kujiamini zaidi pasipo kuwa na hofu katika kukabiliana na ugonjwa
huo.
Aidha, amebainisha kuwa Hospitali hiyo imejipanga
kikamilifu kwa ajili ya kutoa huduma endapo mgonjwa yeyote atabainika kuwa na
ugonjwa huo. “Tunalo eneo la kuwahifadhi wagonjwa wanaoshukiwa kuwa na homa ya
nyani, na tutawahudumia kwa kushirikiana na mamlaka husika,”
Wananchi wametakiwa kuwa waangalifu na kuchukua
tahadhari kwa kuepuka kugusana na mtu anayeshukiwa kuwa na dalili za ugonjwa
huo, kutochukua vitu alivyogusa, na kuhakikisha wananawa mikono mara kwa mara
ili kuepuka maambukizi.
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga inaendelea
kufuatilia kwa karibu hali ya maambukizi ya homa ya nyani na kuwahimiza
wananchi kufika kwenye vituo vya afya endapo watapata dalili zinazoshukiwa kuwa
za ugonjwa huo.
Daktari Godfrey Maige kutoka Idara ya Magonjwa ya
Ndani katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga akiwasilisha mada ya
ugonjwa wa homa ya nyani (Mpox) leo Machi 19, 2025.
Daktari bingwa wa Magonjwa ya dharura Dkt. Patrick Venance akizungumza.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Shinyanga, Dkt. Luzila John, akizungumza leo Machi 19, 2025.
Post a Comment