" TANZANIA KUENDELEA KUUNGA MKONO JITIHADA ZA KIKANDA ZA KUTAFUTA AMANI MASHARIKI MWA DRC

TANZANIA KUENDELEA KUUNGA MKONO JITIHADA ZA KIKANDA ZA KUTAFUTA AMANI MASHARIKI MWA DRC





Tanzania itaendelea kuunga mkono jitihada za kikanda na kimataifa zinazoendelea katika kutafuta amani ya kudumu katika eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Hayo yameelezwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thatib Kombo wakati akizungumza kuhusu Mkutano wa Pamoja wa Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika Harare, Zimbabwe, Machi 17, 2025 kwa lengo la kujadili hali ya amani na usalama katika eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Mhe. Waziri Kombo ambaye ameongoza ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huo amesema, Tanzania tangu enzi za Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere imekuwa mstari wa mbele katika kutafuta suluhu ya migogoro katika nchi mbalimbali kwa njia za amani na zinazofuata misingi ya kidiplomasia na kusisitiza umuhimu wa kutekeleza kikamilifu maazimio yote yanayofikiwa kwenye mikutano ya aina hiyo ili kuwa na kanda salama kwa maslahi mapana ya raia wake.

Amesema Tanzania kama Mwenyekiti wa Asasi ya SADC ya Siasa, Ulinzi na Usalama itaendelea kutekeleza jukumu lake kubwa la kuhakikisha amani na usalama katika kanda vinadumishwa na kurejeshwa katika maeneo ambayo yana migogoro ikiwemo eneo hilo la Mashariki mwa DRC.

“Nampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Asasi ya SADC ya Siasa, Ulinzi na Usalama, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuja na pendekezo la kuziunganisha Jumuiya hizi kubwa za kikanda yaani EAC na SADC ili kwa pamoja kutafuta suluhu ya kudumu katika eneo hilo na tunaunga mkono mchakato wa kutafuta amani wa Luanda na ule wa Nairobi, alisema Mhe. Waziri Kombo.

Ameongeza kusema, Mkutano huo pamoja na kutathmini jitihada mbalimbali za kikanda zinazoendelea katika kutafuta suluhu ya mgogoro huo unaoendelea mashariki mwa Congo, lakini pia umeazimia kutekeleza makubaliano yote yatakayofikiwa ili kuhakikisha wananchi katika eneo la Mashariki mwa Congo wanakuwa salama na kuendelea na shughuli zao za kila siku kama kawaida.

Mkutano huo umeongozwa kwa ushirikiano kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa EAC, Mhe. Dkt. Musalia Mudavadi pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara za Kimataifa wa Zimbabwe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa SADC, Mhe. Prof. Amon Murwira.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Mhe. Prof. Murwira amesisitiza umuhimu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya zote mbili kujitoa kwa hali na mali na kuwa na utashi wa kisiasa katika kuhakikisha makubaliano yanayofikiwa yanatekelezwa.

Mkutano huo pamoja na mambo mengine umejadili pia namna ya upatikanaji wa rasilimali na fedha katika kuchangia jitihada za kutafuta amani katika eneo la mashariki mwa Congo.

Ujumbe wa Tanzania ulimjumuisha pia Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Luteni Jenerali Salum Haji Othman ambaye alimwakilisha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda na Meja Jenerali Ibrahim Mhona, Mkuu wa Operesheni na Mafunzo Jeshini na Viongozi Waandaizi kutoka Serikalini.

Post a Comment

Previous Post Next Post