Na Mapuli Kitina Misalaba
Mkoa wa Shinyanga umeendelea kuwa miongoni mwa mikoa
inayoathiriwa zaidi na ugonjwa wa malaria, huku kiwango cha maambukizi kikiwa
asilimia 16, ambacho ni mara mbili ya wastani wa kitaifa.
Mratibu wa Malaria Mkoa wa Shinyanga, Betty Shayo,
amesema kuwa takwimu hizo zinahusisha watoto wenye umri chini ya miaka mitano,
ambapo kati ya watoto 100, watoto 16 wanapatikana na vimelea vya malaria,
ikilinganishwa na wastani wa kitaifa ambapo watoto 8 kati ya 100 hugundulika na
ugonjwa huo.
"Hii
asilimia ni kubwa ukilinganisha na wastani wa kitaifa, hivyo inathibitisha kuwa
Mkoa wetu unaushamili mkubwa wa malaria,"
amesema.
Kwa mujibu wa Shayo, juhudi mbalimbali zinaendelea
ili kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo, ikiwemo kuhakikisha upimaji na tiba ya
malaria vinapatikana bure kwa wananchi wote.
"Mkakati
wetu wa kwanza ni tiba na upimaji wa malaria. Huwezi kupewa dawa za malaria
bila kupima, na tunasisitiza kuwa upimaji na matibabu ya malaria ni bure,"
ameongeza.
Aidha, amewataka wananchi kuzingatia matumizi ya
vyandarua kila siku ili kujikinga na maambukizi ya malaria.
"Ukishachukua
chandarua chako hakikisha unakitumia kila usiku. Usilale bila kutumia chandarua
kwa sababu ndicho kinga madhubuti dhidi ya mbu waenezao malaria,"
amesisitiza.
Wakati huo huo, zoezi la ugawaji wa vyandarua linaendelea mkoani Shinyanga, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kupunguza maambukizi ya malaria na kuwakinga wananchi dhidi ya ugonjwa huo.
Post a Comment