Na Lucas Raphael, Misalaba Media,Tabora
Wajasiliamali 500 wanaoishi pembezoni mwa hifadhi katika mikoa ya Kanda ya magharibi ya Tabora na Katavi wamewezeshwa vitendea kazi vya kuchumia,kukaushia na kuhifadhia uyoga mwitu unaoliwa na binadamu vyenye gharama shilingi Milioni 260.
Msaada huo umetolewa na wadau wa mazingira kwa lengo la kuwasaidia Wajasiliamali hao kujiingizia kipato kupitia uzalishaji na uuzaji wa zao la uyoga badala ya kutegemea rasilimali za misitu zinazoathiri Mazingira.
Akizungumza katika warsha kuhusu zao la uyoga iliyofanyika ukumbi wa Isike Mwanakiyungi mkoani Tabora, meneja mradi wa shirika hilo Romanus Mwakimata alisema kwa kipindi cha miaka 4 ya mwanzo waliweza kufikia vikundi 30 vyenye watu 500 na kuwapatia vifaa hivyo ambavyo ni makaushio ya uyoga na mboga za asili 34 katika vijiji 30 vilivyopo kwenye mikoa hiyo .
Mwakimata alitaja vifaa vingine kuwa ni vikapu vya asili 2,000 na vitabu 3,000 vya mafunzo kuhusu uyoga kwa ajili ya kuongeza mnyororo wa thamani ya uyoga mwitu unaoliwa na binadamu..
Alisema mradi una lengo la kutoa mafunzo kwa waokotaji na kulinda ubora wa asili ya uyoga na kuwaunganisha na masoko ili kuboresha na kuimarisha uhakika wa soko la uyoga.
Aidha Mwakimata alisema kwamba nia na mathumuni ni kushirikisha wadau katika kuboresha mnyororo wa thamani wa zao la uyoga .
Hata hivyo aliitaka mamlaka ya uthibiti ubora TBS iweze kuthibiti ubora wa uyoga ili uweze kuaminika katika masoko mbalimbali na walaji
Sanjari la hilo waliomba serikali na sekta binafsi kuwashawishi wadau mbalimbali ili kuweza kupunguza vikwazo katika uendeshaji Masoko ya uyoga
Awali akifungua warsha hiyo Mkuu wa Mkoa wa Tabora Paul Matiko Chacha, amewataka Wananchi wanaotoka ndani na nje ya Mkoa wa Tabora kutumia fursa ya Warsha ya Kitaifa ya Uyoga Mwitu Unaoliwa na Binadamu, kupata uzoefu na uwezeshwaji katika kukuza mnyororo wa thamani wa uyoga mwitu unaoliwa kama chakula, dawa za jadi na chanzo cha mapato.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora akiwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Cornel Magembe, alisema kutokana na changamoto zinazoikabili sekta hii ya kukuza uyoga mwitu unaoliwa amewaasa washiriki kutumia fursa ya jukwaa hilo kupata utaalamu, uzoefu na ubunifu katika kufungua njia na kukuza sekta ya uyoga nchini.
Alibainisha kuwa waandaji wa mradi huo kuwaandaa washiriki wa Warsha ya Uyoga Mwitu Unaoliwa na Binadamu, kwa kuwawezesha katika uvunaji, kuwajengea uwezo na kuwawezesha katika upatikanaji wa masoko na kuimarisha mnyororo wa thamani wa sekta hiyo.
Aidha Magembe alitoa wito kwa TAFORI kuendelea na Utafiti na utambuzi na uzalishaji wa uyoga mwitu wa aina mbalimbali kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wake kwa uhakika wa chakula nchini na kushirikisha matokeo katika warsha za umma.
Mradi huo ulioanzishwa na ADAP, Adansonia Consulting kwa kushirikiana na TAFORI unaoendana na dira ya Taifa ya mwaka 2025 “Tanzania version 2025” na Mkakati wa Kitaifa wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini “The National Strategy for Growth and Deduction of Poverty” unatarajiwa kufungua fursa za kiuchumi na kukuza mnyororo wa thamani wa sekta ya uyoga mwitu unaoliwa nchini.
Mwisho
Post a Comment