Na Daniel Sibu, Misalaba Media
Katika kusherehekea Siku ya Mwanamke Duniani, walimu wanawake wa Mkoa wa Shinyanga kupitia Chama cha Walimu (CWT) wamefanya maadhimisho yenye nguvu, hamasa, na motisha kwa wanawake katika sekta ya elimu.
Mgeni rasmi katika sherehe hiyo ni Afisa Elimu Taaluma wa Mkoa wa Shinyanga, Bi. Fausta Luoga, ambaye ametoa ujumbe wenye msukumo mkubwa kwa wanawake wote.
Katika hotuba yake, Bi. Fausta amesisitiza umuhimu wa wanawake kujitambua, kujituma, na kujiamini katika kila nyanja ya maisha yao, hasa katika taaluma ya ualimu.
“Wanawake tunapaswa kujiamini katika nafasi zetu, kazi zetu, na kuwa mabalozi wa wenzetu. Najua wengi tunapitia changamoto mbalimbali, ikiwa ni pamoja na msongo wa mawazo na hata matatizo ya madeni. Hata hivyo, hatupaswi kukubali kufanywa vyombo vya kupokea rushwa za ngono ili kupata fursa fulani. Ofisi yangu imeanzisha kampeni madhubuti ya kupambana na changamoto hizi na tutahakikisha zinakomeshwa kabisa,” alisisitiza.
Ametoa pongezi kwa walimu wanawake wanaoonyesha mfano bora wa uongozi, akimtaja Bi. Stella Halimoja, Mkuu wa Shule ya Msingi Lubaga, ambaye ameiongoza shule yake kwa mafanikio makubwa.
Vilevile, ametoa tumaini kwa walimu wakuu wanawake wa sekondari, akiwahakikishia kuwa mchakato wa kuongeza idadi yao umeanza na kuwataka wafanye kazi kwa bidii na kujiendeleza kitaaluma ili fursa zitakapojitokeza wawe tayari kuzitumia.
Sherehe hiyo pia ilihusisha utoaji wa zawadi kwa walimu wanawake waliotoa mchango mkubwa katika sekta ya elimu:
✅ Madamu Stella Halimoja – Mkuu wa Shule ya Msingi Lubaga, amepata tuzo kwa ufaulu mzuri wa shule yake.
✅ Madamu Leticia Kisima – Mkuu wa Shule ya Shinyanga Girls, amepata tuzo kwa kufanikisha kuondoa alama za sifuri kwa wanafunzi wake.
✅ Mwalimu Theodora Barnaba (Mama Shirima) – Mwanamke shupavu, mpambanaji na mjasiriamali amepewa tuzo maalum ya ujasiri.
Sherehe hiyo pia imehusisha kumuaga aliyekuwa Katibu wa CWT Wilaya, Bi. Rose Lesha Rwechungula, ambaye amehamia Bukombe.
Amekumbukwa kwa mchango wake mkubwa, na ameondoka na zawadi maalum pamoja na nyimbo za kwaya ya walimu.
Katibu wa sasa wa CWT Wilaya, Bi. Rose Mboneko, ndiye aliyeratibu hafla hiyo kwa mafanikio makubwa, na imehudhuriwa pia na Afisa Elimu Msingi, Bi. Mary Maka.
Hata walimu wanaume wameshiriki, ikiwa ni sehemu ya kuonesha mshikamano na upendo kwa wenzao wa kike.
Katika hitimisho, walimu wamehamasishwa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa CWT na uchaguzi mkuu ujao, huku wakihimizwa kuwa mabalozi wa kuisemea vyema serikali na rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Post a Comment