" WASIRA AHITIMISHA ZIARA YAKE MKOANI SHINYANGA, ATOA MAAGIZO KWA WAKANDARASI NA WASIMAMIZI WA MRADI WA UWANJA WA NDEGE SHINYANGA

WASIRA AHITIMISHA ZIARA YAKE MKOANI SHINYANGA, ATOA MAAGIZO KWA WAKANDARASI NA WASIMAMIZI WA MRADI WA UWANJA WA NDEGE SHINYANGA

Na Mapuli Kitina Misalaba

Mradi wa upanuzi na ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Shinyanga umefikia asilimia 75 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Juni 2025.

Akisoma taarifa ya maendeleo ya mradi huo kwa niaba ya Meneja wa TANROADS, Mhandisi Chiambo Matoke, mmoja wa wasimamizi wa mradi amesema kuwa kazi inaendelea vizuri huku gharama ya mradi zikifikia zaidi ya Bilioni 48.

Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira, ametembelea uwanja huo na kuwataka wakandarasi na wasimamizi kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati ili uanze kutoa huduma stahiki kwa wananchi.

Pia Wasira ametembelea mradi huo pamoja na kufanya mazungumzo na viongozi na wanachama wa CCM katika Wilaya ya Kishapu.

Katika ziara hiyo, Wasira amesisitiza kuwa viongozi wanaochaguliwa kupitia CCM wanapaswa kuwatumikia wananchi bila kujali itikadi ya vyama, dini wala kabila.

Aidha, ametumia nafasi hiyo kutoa onyo kali dhidi ya vitendo vya rushwa, hasa kwa wale wanaotarajia kugombea nafasi mbalimbali, ikiwemo ubunge na udiwani.

“Kuna watu wameanza kutafuta wajumbe wao kwa kununua kura kwa elfu 20, lengo lao ni kuja kugombea. Sasa niwahimize wananchi, wakiwapa hiyo hela, nyie ipokeeni lakini kwenye sanduku la kura hakikisheni mnampigia kiongozi anayefaa kuwatumikia wananchi,” amesema Wasira.

Ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kuwa makini na viongozi wanaojaribu kununua uongozi kwa fedha badala ya kuonyesha uwezo wa kutatua changamoto za wananchi.

“Msichague viongozi kwa sababu wamewapa elfu 20. CCM tunataka viongozi wanaoweza kuwatumikia wananchi bila kujali itikadi zao, na hivyo ndivyo tumekuwa tukifanya tangu zamani. Ndiyo maana tunakubalika na tutaendelea kuwatumikia wananchi,” amesema Wasira .

Mbunge wa Jimbo la Kishapu, Mhe. Boniphace Butondo, amesema kuwa ndani ya miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, jimbo hilo limepokea fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, hatua inayothibitisha dhamira ya serikali ya kuwaletea wananchi maendeleo.

Butondo amemshukuru Rais Samia kwa juhudi zake kubwa za kuimarisha sekta mbalimbali jimboni humo na kuahidi kuwa katika uchaguzi mkuu wa 2025, wananchi wa Kishapu watamrudishia kura za kishindo kama ishara ya kuthamini kazi anayofanya.

Hata hivyo, Butondo ameeleza kuwa bado kuna changamoto kadhaa zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo, ikiwemo upatikanaji wa maji safi na salama kutoka Ziwa Victoria.

Amesema wananchi wa kata mbalimbali bado wanakabiliwa na uhaba wa maji safi, hali inayowalazimu kutumia vyanzo visivyo salama kwa afya, hivyo akaiomba serikali kuharakisha upatikanaji wa maji hayo.

Aidha, Mbunge huyo ametaja changamoto ya miundombinu, akibainisha kuwa barabara inayotoka Kata ya Kolandoto kuelekea Kishapu inahitaji kuboreshwa kwa kiwango cha lami ili kuimarisha usafiri na kurahisisha mawasiliano ya wananchi wa maeneo hayo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mabala Mlolwa, amempongeza Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira, kwa kufanya ziara yake mkoani Shinyanga na kutoa mwelekeo wa chama kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025.

Mlolwa amesema kuwa CCM mkoani Shinyanga inaendelea kuwa imara na kujipanga kuhakikisha chama hicho kinapata kura nyingi kwa wagombea wake katika uchaguzi huo.

Amesema chama kimejipanga kuandaa wagombea bora, wenye kukubalika kwa wananchi, ili kuhakikisha wanatekeleza kwa ufanisi ilani ya CCM na kuendelea kuwaletea wananchi maendeleo.

Wasira amehitimisha ziara yake ya siku tatu mkoani Shinyanga leo Machi 28, 2025 na ametangaza kuwa ataendelea na ziara yake kesho mkoani Simiyu.

Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira, baada ya kuwasili katika uwanja wa Ndege Shinyanga ikiwa ni sehemu ya ziara yake leo Machi 28, 2025.


 

Post a Comment

Previous Post Next Post