
Na Mapuli Kitina Misalaba
Makamu
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Ndg. Stephen Masato Wasira, amewasili mkoani Shinyanga kwa ajili
ya ziara ya siku tatu kuanzia leo, akilenga kuimarisha chama na kujadiliana na
wanachama kuhusu masuala ya maendeleo na mwelekeo wa CCM.
Wasira alipokelewa
katika ofisi ya CCM Mkoa wa Shinyanga kabla ya kuelekea kwenye mkutano wa
hadhara uliofanyika katika ukumbi wa
mikutano wa Lyakale, mjini Shinyanga.
Katika
mkutano huo, viongozi wa chama na wananchi wamepata nafasi ya kueleza
changamoto mbalimbali zinazowakabili, huku Wasira akitoa maagizo kwa viongozi wa
mkoa kushughulikia matatizo hayo kwa haraka.
Katika
mkutano huo, viongozi kutoka kata mbalimbali na wawakilishi wa wananchi wamebainisha
changamoto kadhaa zinazoikabili jamii ya Shinyanga, ikiwa ni pamoja na Ukamilishaji wa Soko Kuu la Mkoa wa
Shinyanga ambapo wananchi wameendelea kulalamikia ucheleweshwaji wa
ukamilishaji wa Soko Kuu la Mkoa wa
Shinyanga, wakisema kuwa mradi huo umekuwa ukiboreshwa kwa zaidi ya
miaka miwili bila kukamilika.
Hali hiyo
imesababisha wafanyabiashara wengi kufanya kazi katika mazingira magumu, huku
wengine wakilazimika kuhifadhi bidhaa zao kwenye maeneo yasiyo rasmi.
Pia ubovu wa Barabara ya Wawaza ambapo wananchi wameeleza
kero ya ubovu wa barabara inayotoka
mjini Shinyanga kuelekea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga (Wawaza).
Wamesisitiza
kuwa hali mbaya ya barabara hiyo inasababisha usumbufu mkubwa kwa wagonjwa na
wananchi wanaohitaji huduma hospitalini ambapo wameiomba serikali kuboresha
barabara hiyo kwa kiwango cha lami ili kurahisisha usafiri na kupunguza athari
zinazojitokeza.
Kero nyingine ni upungufu wa Huduma za Afya ambapo wakazi wa
Kata ya Ngokolo wameeleza changamoto ya ukosefu wa kituo cha afya, wakiiomba
serikali kujenga kituo hicho ili kupunguza umbali na usumbufu wa kupata
matibabu.
Akijibu
hoja hizo, Makamu Mwenyekiti wa CCM
Tanzania Bara, Ndg. Stephen Wasira, amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga
kuhakikisha changamoto hizo zinashughulikiwa kwa haraka ili wananchi waendelee
na shughuli zao bila vikwazo.
Aidha,
Wasira ametumia fursa hiyo kueleza kuwa CCM
si chama cha msimu wala chama cha uchaguzi, bali ni chama chenye mizizi
imara kinachotumikia wananchi wakati wote.
Amesema
kuwa chama hicho kitaendelea kuwasikiliza wananchi na kuhakikisha changamoto
zinazowakabili zinapatiwa ufumbuzi.
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira, ametumia nafasi hiyo kuwataka wananchi
kuepuka vyama vya siasa vinavyohamasisha vurugu na kuhatarisha amani ya nchi
kwa maslahi binafsi.
Akizungumza katika ziara yake mkoani
Shinyanga, Wasira amesema Tanzania ni nchi yenye utulivu na mshikamano, hivyo
ni wajibu wa kila Mtanzania kuilinda na kuienzi amani hiyo kwa kuepuka siasa za
chuki na migawanyiko.
Katika
ziara yake, Wasira pia amezindua ofisi
mpya ya CCM Kata ya Chibe, akisisitiza kuwa ofisi hiyo inapaswa kutumika
ipasavyo kwa ajili ya kusuluhisha changamoto za wananchi, ikiwa ni pamoja na
migogoro ya ardhi na wakulima.
Amewataka
viongozi wa chama kutumia ofisi hizo kama nyenzo ya kuimarisha mshikamano ndani
ya CCM na kushughulikia mahitaji ya wananchi kwa haraka.
Mwenyekiti
wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mabala
Mlolwa, amesema kuwa mkoa huo umeshakamilisha maandalizi kuelekea
uchaguzi mkuu wa 2025.
Amesisitiza
kuwa CCM inatarajia ushindi mkubwa kwa
Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na mgombea mwenza wake, Balozi Dkt. Emmanuel
Nchimbi, katika uchaguzi huo.
Mlolwa
alimshukuru Wasira kwa kufanya ziara mkoani humo na kumhakikishia kuwa CCM Mkoa wa Shinyanga iko imara na
itaendelea kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha chama hicho kinapata ushindi wa
kishindo.
Makamu
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Ndg. Stephen Masato Wasira, akizungumza kwenye mkutano wake mjini
Shinyanga leo Machi 26, 2025.
Makamu
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Ndg. Stephen Masato Wasira, akizungumza kwenye mkutano wake mjini
Shinyanga leo Machi 26, 2025.
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Ndg. Stephen Masato Wasira, akijibu maswali yaliyoulizwa kwenye mkutano huo.
Mwenyekiti
wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mabala
Mlolwa, akizungumza kwenye mkutano huo leo Machi 26, 2025
Mwenyekiti
wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mabala
Mlolwa, akizungumza kwenye mkutano huo leo Machi 26, 2025
Post a Comment