" WASIRA AWATAKA WANANCHI KULINDA AMANI YA TAIFA AWASISITIZA KUPUUZA VYAMA VINAVYOHAMASISHA VURUGU

WASIRA AWATAKA WANANCHI KULINDA AMANI YA TAIFA AWASISITIZA KUPUUZA VYAMA VINAVYOHAMASISHA VURUGU

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Ndg. Stephen Masato Wasira, akizungumza kwenye mkutano wake mjini Shinyanga leo Machi 26, 2025.

Na Mapuli Kitina Misalaba

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Ndg. Stephen Masato Wasira, amewasili mkoani Shinyanga kwa ajili ya ziara ya siku tatu kuanzia leo, akilenga kuimarisha chama na kujadiliana na wanachama kuhusu masuala ya maendeleo na mwelekeo wa CCM.

Wasira alipokelewa katika ofisi ya CCM Mkoa wa Shinyanga kabla ya kuelekea kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Lyakale, mjini Shinyanga.

Katika mkutano huo, viongozi wa chama na wananchi wamepata nafasi ya kueleza changamoto mbalimbali zinazowakabili, huku Wasira akitoa maagizo kwa viongozi wa mkoa kushughulikia matatizo hayo kwa haraka.

Katika mkutano huo, viongozi kutoka kata mbalimbali na wawakilishi wa wananchi wamebainisha changamoto kadhaa zinazoikabili jamii ya Shinyanga, ikiwa ni pamoja na Ukamilishaji wa Soko Kuu la Mkoa wa Shinyanga ambapo wananchi wameendelea kulalamikia ucheleweshwaji wa ukamilishaji wa Soko Kuu la Mkoa wa Shinyanga, wakisema kuwa mradi huo umekuwa ukiboreshwa kwa zaidi ya miaka miwili bila kukamilika.

Hali hiyo imesababisha wafanyabiashara wengi kufanya kazi katika mazingira magumu, huku wengine wakilazimika kuhifadhi bidhaa zao kwenye maeneo yasiyo rasmi.

Pia ubovu wa Barabara ya Wawaza ambapo wananchi  wameeleza kero ya ubovu wa barabara inayotoka mjini Shinyanga kuelekea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga (Wawaza).

Wamesisitiza kuwa hali mbaya ya barabara hiyo inasababisha usumbufu mkubwa kwa wagonjwa na wananchi wanaohitaji huduma hospitalini ambapo wameiomba serikali kuboresha barabara hiyo kwa kiwango cha lami ili kurahisisha usafiri na kupunguza athari zinazojitokeza.

Kero nyingine ni upungufu wa Huduma za Afya  ambapo wakazi wa Kata ya Ngokolo wameeleza changamoto ya ukosefu wa kituo cha afya, wakiiomba serikali kujenga kituo hicho ili kupunguza umbali na usumbufu wa kupata matibabu.

Akijibu hoja hizo, Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Ndg. Stephen Wasira, amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kuhakikisha changamoto hizo zinashughulikiwa kwa haraka ili wananchi waendelee na shughuli zao bila vikwazo.

Aidha, Wasira ametumia fursa hiyo kueleza kuwa CCM si chama cha msimu wala chama cha uchaguzi, bali ni chama chenye mizizi imara kinachotumikia wananchi wakati wote.

Amesema kuwa chama hicho kitaendelea kuwasikiliza wananchi na kuhakikisha changamoto zinazowakabili zinapatiwa ufumbuzi.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira, ametumia nafasi hiyo kuwataka wananchi kuepuka vyama vya siasa vinavyohamasisha vurugu na kuhatarisha amani ya nchi kwa maslahi binafsi.

Akizungumza katika ziara yake mkoani Shinyanga, Wasira amesema Tanzania ni nchi yenye utulivu na mshikamano, hivyo ni wajibu wa kila Mtanzania kuilinda na kuienzi amani hiyo kwa kuepuka siasa za chuki na migawanyiko.

Katika ziara yake, Wasira pia amezindua ofisi mpya ya CCM Kata ya Chibe, akisisitiza kuwa ofisi hiyo inapaswa kutumika ipasavyo kwa ajili ya kusuluhisha changamoto za wananchi, ikiwa ni pamoja na migogoro ya ardhi na wakulima.

Amewataka viongozi wa chama kutumia ofisi hizo kama nyenzo ya kuimarisha mshikamano ndani ya CCM na kushughulikia mahitaji ya wananchi kwa haraka.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mabala Mlolwa, amesema kuwa mkoa huo umeshakamilisha maandalizi kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025.

Amesisitiza kuwa CCM inatarajia ushindi mkubwa kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na mgombea mwenza wake, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, katika uchaguzi huo.

Mlolwa alimshukuru Wasira kwa kufanya ziara mkoani humo na kumhakikishia kuwa CCM Mkoa wa Shinyanga iko imara na itaendelea kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha chama hicho kinapata ushindi wa kishindo.

Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali, wakiwemo:Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Anamringi Macha, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mhe. Anord Makombe, Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Mhe. Paschal Patrobas Katambi, Viongozi wa CCM ngazi za kata na wilaya, viongozi wa taasisi mbalimbali na Wadau wa maendeleo.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Ndg. Stephen Masato Wasira, akizungumza kwenye mkutano wake mjini Shinyanga leo Machi 26, 2025.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Ndg. Stephen Masato Wasira, akizungumza kwenye mkutano wake mjini Shinyanga leo Machi 26, 2025.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Ndg. Stephen Masato Wasira, akijibu maswali yaliyoulizwa kwenye mkutano huo.




 

Post a Comment

Previous Post Next Post