Na WMJJWM – Geita.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amewahimiza wanawake kushiriki kwa wingi katika sekta ya madini kama njia ya kuwawezesha kiuchumi na kuchochea maendeleo ya Taifa.
Akizungumza katika Kongamano la Kuelekea Siku ya Wanawake Duniani la Kanda ya Ziwa lililofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Ushirombo, Wilaya ya Bukombe, mkoani Geita, Dkt. Gwajima amesema wanawake wanachangia kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa nchi kupitia sekta hiyo na wanapaswa kupata fursa sawa za kumiliki na kuendeleza shughuli zao.
“Ni ukweli usiopingika kuwa wanawake wanachangia pakubwa katika uchumi wa nchi kupitia sekta ya madini. Hivyo, ni muhimu kuhakikisha wanapata fursa sawa za kumiliki na kuendeleza shughuli zao ili kujipatia kipato na kukuza uchumi wa familia na jamii kwa ujumla” amesema Dkt. Gwajima.
Amefafanua kuwa mada kuu ya kongamano hilo ni Ushiriki na Nafasi ya Mwanamke kwenye Maendeleo ya Sekta ya Madini ikilenga kuhamasisha wanawake kushiriki zaidi katika sekta hiyo, hususan kwa Kanda ya Ziwa, ambapo tayari Mkoa wa Geita una vikundi 43 vya wanawake vinavyomiliki leseni za uchimbaji madini na vikundi vingine 20 vilivyopatiwa vitalu vya madini.
Katika kongamano hilo, Dkt. Gwajima ameeleza changamoto zinazowakumba wanawake wanaojihusisha na uchimbaji na uchakataji wa madini, ikiwemo upungufu wa vifaa vya kuchakata madini, mitaji pamoja na elimu.
Dkt Gwajima ameahidi kuzitatua changamoto hizo kwa kuziunganisha na zingine zote kutoka Kanda zote saba za makongamano Ili, kushirikisha sekta zote husika kwa ajili ya kuzitafutia ufumbuzi kwa kushirikiana na wakuu wa mikoa husika.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martine Shigela, amemshukuru Waziri Gwajima kwa kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika sekta ya madini na kusikiliza changamoto zao.
Shigella ameahidi kuhakikisha changamoto zote zilizotolewa katika kongamano hilo zinakusanywa na kufanyiwa kazi ili kutoa suluhisho la kudumu kwa wanawake wa Kanda ya Ziwa.
Post a Comment