Na Halima Issa, Misalaba Media
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amemuelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Mhandisi Balozi Aisha Amour, kuwasimamisha kazi wasimamizi wote wa Mizani waliokuwa zamu katika Mizani zilizopo katika barabara kuu ya T1 inayoanzia Dar es Salaam – Zambia kupitia mpaka wa Tunduma kwa ajili ya kupisha uchunguzi wa malalamiko katika Mizani hizo.
Ulega amefanya maamuzi hayo mara baada ya kadhia iliyojitokeza hivi karibuni kwa msafirishaji Bi. Pamela James Bukumbi mwenye gari ya mizigo namba T 137 DLQ likiwa na tela T 567 CUR iliyotokea katika kituo cha Mizani ya Vigwaza akilalamika kuhusu kutozwa faini ya kuzidisha uzito katika Mizani hiyo wakati mizani nyingine alizopita gari yake haikuwa imezidisha uzito.
Ulega ametoa maelekezo hayo jijini Dodoma leo tarehe 20 Machi, 2025 mara baada ya kupata taarifa hiyo na kusikiliza pande zote mbili kutoka kwa mlalamikaji na mlalamikiwa ambaye ni Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na kubaini kuwa lipo tatizo la wazi ambalo limesababisha kadhia hiyo na kutoa maelekezo makuu matano.
“Baada ya kugundua liko tatizo, Nimeamua kuchukua hatua zifuatazo moja ni kuwasimamisha wale wasimamizi wetu wa Mizani wa hii T1 barabara nzima kuanzia Tunduma mpaka inafika pale Vigwaza waliokuwa kwenye zamu kwa siku ile wakati tukio linatokea”, amesema Ulega.
Ulega ameeleza kuwa amewasimamisha wasimamizi hao kwa lengo la kufanya uchunguzi ambapo tayari timu ya wataalam ya kuchunguza tukio hilo imeundwa ili kufuatilia safari nzima ya gari hilo ili kupata hali halisi na kuwasilisha mapendekezo mengine ili hatua za kinidhamu ziweze kuchukuliwa dhidi ya wale wote ambao watabainika na vitendo visivyoridhisha.
Post a Comment