
Na Mapuli Kitina Misalaba
Katibu wa Jumuiya ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Kanda ya Ziwa, Bwana Daniel Kapaya, amefanya ziara katika ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita (RPC), SACP Safia Jongo, na kujadili hatua za kupambana na ukatili wa kijinsia unaoendelea kushamiri katika jamii.
Katika mazungumzo hayo, Kapaya ameonyesha wasiwasi wake juu ya kuongezeka kwa matukio ya ukatili dhidi ya watoto, wanawake, wanaume, na makundi maalum, akisema kuwa ukatili umekuwa janga la kitaifa.
Ameeleza kuwa sehemu nyingi zenye shughuli za uchumi kama migodi na maeneo ya uvuvi, ukatili wa kijinsia hufanyika kwa siri, huku waathirika wakihofia kutoa taarifa kwa vyombo vya dola.
"Uhalifu mkubwa unatokea pale jamii inapokuwa wasiri. Wananchi wanapaswa kutoa taarifa za ukatili badala ya kufumbia macho matendo haya mabaya, kwani kukaa kimya ni sawa na kushiriki uhalifu huo," amesema Kapaya.
Katibu huyo pia amemshukuru Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, SACP Safia Jongo, kwa kushirikiana na SMAUJATA Mkoa wa Geita katika kupambana na ukatili. Amesema juhudi za jeshi la polisi ni muhimu katika kuhakikisha matukio ya ukatili yanapungua kwa kuwachukulia hatua wahusika na kutoa elimu kwa jamii.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, SACP Safia Jongo, amepongeza kazi kubwa inayofanywa na SMAUJATA katika kupaza sauti dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Amesema jeshi la polisi linaendelea kushirikiana na mashirika na wadau mbalimbali kuhakikisha ukatili unapigwa vita kwa nguvu zote.
Ameeleza kuwa matukio mengi ya ukatili yanayoripotiwa mkoani Geita hutokana na wivu wa kimapenzi, watoto kulawitiwa na kubakwa, familia kushindwa kutoa taarifa za ukatili unaofanyika majumbani, na baadhi ya watu kujichukulia sheria mkononi. Pia ametaja ukatili wa mama wa kambo kama moja ya changamoto zinazohitaji juhudi za pamoja kupambana nazo.
"Elimu juu ya madhara ya ukatili inapaswa kufika kila mahali, siyo tu kwenye mikutano ya hadhara, bali hadi kwenye nyumba za ibada kama makanisa na misikiti ili kuhakikisha jamii inakuwa na uelewa mpana wa haki na wajibu wao," amesema SACP Jongo.
Katika ziara hiyo, Katibu wa SMAUJATA Kanda ya Ziwa, Bwana Daniel Kapaya, ameambatana na viongozi wa SMAUJATA Mkoa wa Geita, ambao pia walishiriki katika mazungumzo hayo na kuahidi kuendelea kushirikiana na jeshi la polisi katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia mkoani humo.
Mazungumzo kati ya SMAUJATA na Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita yanaashiria hatua kubwa katika kupambana na ukatili wa kijinsia, huku pande zote zikiahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu.
Pamoja na changamoto zilizopo, ushirikiano kati ya mashirika ya kijamii na vyombo vya dola unatajwa kuwa silaha muhimu katika kufanikisha vita dhidi ya ukatili na kuhakikisha jamii inakuwa mahali salama kwa kila mtu.
Post a Comment