Na Respice Swetu, Misalaba Media -Kasulu
Mkazi wa
halmashauri ya mji wa Kasulu Wencheslaus Luyaga maarufu kwa jina la Gadafi ambaye
mwishoni mwa mwaka jana alisafiri kwa kutumia usafiri wa baiskeli kutoka Kasulu
hadi Dodoma kuunga mkono juhudi za Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika
kuwaletea maendeleo wananchi, amefanya safari nyingine ya kutoka Kasulu mpaka Tabora
kuhamasisha utalii wa ndani.
Akizungumzia
safari hiyo, Gadafi ambaye ni mwalimu mkuu wa shule ya msingi Junga iliyopo halmashauri
ya mji wa Kasulu amesema, maamuzi ya kuibeba ajenda hiyo, yamechagizwa na mafanikio
yaliyopatikana katika sekta ya utalii nchini baada ya Rais wa Jamhuri ya
Muuungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kuuhamasisha umma na dunia kwa
ujumla kuhusu fursa za utalii zilizopo nchini.
Gadafi
aliyeipa safari hiyo jina la “utalii wa magharibi”,
anatarajia kuikamilisha mwishoni mwa wiki kwa kupita katika maeneo mbalimbali
ya utalii na uhifadhi yaliyopo kwenye mikoa ya Tabora na Kigoma ambako pia
atakuwa anazungumza na viongozi mbalimbali wa maeneo hayo.
Sanjari na utalii
huo, malengo mengine ya “safari ya magharibi” ni kuwahamasisha wananchi
kushiriki katika uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani utakaofanyika Oktoba
mwaka huu, kuilinda amani ya Tanzania na uzingatifu katika utunzaji wa afya kwa
makundi maalumu hususan watoto, kina mama na watu wenye ulemavu.
Gadafi ambaye
katika siku za karibuni amejipatia umaarufu mkubwa kutokana na kutumia usafiri
wa baiskeli kwenda maeneo mbalimbali ya nchi akiwa amebeba bendera ya halmashauri
ya mji wa Kasulu na ajenda za kitaifa, amedhamiria kuendelea na utaratibu huo ili
kuyafikia maeneo mengi zaidi.
Post a Comment