Askofu mteule wa Jimbo Katoliki Iringa Romanus Elamu Mihali, kesho Jumapili tarehe 27.04.2025 atawekwa wakfu na kusimikwa rasmi kuwa Askofu mpya wa Jimbo la Iringa.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa, Misa ya utolewaji wa Daraja la Uaskofu itaanza saa 3:00 asubuhi katika uwanja wa Senta ya Vijana mjini Iringa, na itaongozwa na Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, ambaye atasaidiana na maaskofu wengine wawili.
Askofu mteule Mihali aliteuliwa kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Iringa na Hayati Baba Mtakatifu Fransisko mnamo tarehe 28.01.2025, baada ya kuridhia ombi la kustaafu kwa mujibu wa sheria za Kanisa kwa aliyekuwa Askofu wa Jimbo hilo Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa.
Askofu Mteule Mihali alizaliwa mnamo Juni 10 mwaka 1969 katika Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa.
Baada ya kumaliza masomo yake ya kipadre, alipewa Daraja takatifu la Upadre mnamo Julai 13 mwaka 2000, ambapo alihudumu katika nafasi mbalimbali Jimboni Iringa.
Alijiendeleza kielimu katika chuo kikuu cha Kerala nchini India na kutunikiwa shahada ya Uzamili katika Sayansi ya wanyama mwaka 2010.
Mpaka kuteuliwa kwake, alikuwa Makamu wa Askofu wa Jimbo Katoliki la Mafinga.
Askofu mteule Mihali atawekwa wakfu na kusimikwa kuwa Askofu wa Jimbo la Iringa licha ya kiti cha kitume kubaki wazi kufuatia kifo cha Baba Mtakatifu Fransisko, kwa kuwa Papa amefariki dunia tayari akiwa amemteua na kutoa hati maalum ya uteuzi ambayo pia inaelekeza namna atakavyopewa Daraja la Uaskofu.
Ikumbukwe kuwa, Mamlaka ya kumteua Padre kuwa Askofu iko kwa Baba mtakatifu pekee, lakini sheria za Kanisa zinampa ruhusa Askofu yeyote wa Kanisa Katoliki kumpa Daraja la Uaskofu Padre aliyeteuliwa kuwa Askofu mbele ya ushuhuda wa Maaskofu wasiopungua wawili, jambo ambalo linapaswa kufanyika baada ya mweka wakfu kuiona hati ya uteuzi kutoka kwa Papa.
Post a Comment